Rais Museveni aeleza ni kwa nini aliunga mkono vita ya kumpindua Mobutu

413
Rais wa Uganda Yoweli Museveni amekanusha kuhusika na wizi wa madini ya DR Congo

Miaka 20 baada ya serikali ya Mobutu Seseseko kupinduliwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ilikuwa inaitwa Zaire, Rais wa Uganda anaeleza ni kwa nini alishiriki vita hiyo.

Rais Yoweli Museveni amesema mkono wake katika vita hiyo ulilenga kuisaidia Rwanda iliyokuwa inavamiwa na waasi wa Interahamwe waliokuwa wamepewa hifadhi na Mobutu.

Museveni amesema haifai kuutafsiri mchango wake katika vita hiyo kama kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine, akisema sababu kubwa ilikuwa waasi hao wa Kinyarwanda.

Mobutu alizaliwa mwaka 1930 na kufariki mwaka 1997. Aliingia madarakani mwaka 1965 na kuiongoza Congo aliyokuja kuiita Zaire kwa muda wa miaka 32.

Interahamwe ni kundi ambalo serikali ya Rwanda inalichukulia kama la kigaidi, na kisheria inakatazwa kuwa na fungamano lolote la kundi hilo ambalo lipo Mashariki mwa Congo.

Ni kundi la wapiganaji ambalo linatuhumiwa kwa utekelezaji wa mauaji ya kimbari yaliyofanyika dhidi ya Watutsi na kugharumi maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja.

Baada ya waasi wa RPF-Inkotanyi kushinda vita ya ukombozi mwaka 1994 na kujihakikishia udhibiti wa nchi, watendaji wa serikali na majeshi walilazimika kutimua mbio.

Wendi wao inaaminika walikimbilia nchini Zaire ambapo Rais Mobutu Seseseko alikuwa amejenga urafiki mkubwa na Rais Habyarimana aliyeuawa wakati ndege yaje inatua, Kigali.

Ndoto ya kujirudishia udhibiti wa Rwanda iliota mizizi tangu walipofika nchini Zaire, na mashambulizi yao ya mara kwa mara yalishuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Rwanda.

Ilibidi majeshi ya Rwanda yaingie nchini Kongo kuwasaka waasi hao ambao walikuwa na uungaji mkono wa Rais Mobutu Seseseko aliyekuja kupinduliwa mnamo Mei 16, 1997.

Rais Museveni wa Uganda hajakanusha kuhusika na vita vya kuwafurusha waasi hao wa Interahamwe na kumng’oa mamlakani Mobutu aliyekuwa anawadhamini.

Akishirikiana na majeshi ya Rwanda, walifanikiwa kumweka madarakani Rais Laurent Desiré Kabila aliyekuja kuuawa katika mazingira ya kutatanisha miaka michache baadaye.

Rais Museveni amenukuliwa na RFI akisema Rwanda ndiyo ilikuwa mstari wa mbele katika vita hiyo, na Uganda ilijihusisha ili kuisaidia Rwanda tu na wala haikuwa na lengo linguine.

Alipoulizwa kama hajavutiwa na madini ya nchi hiyo, alisema kamwe hakuwa na tamaa ya madini hayo, na kusema huo ni uongo ambao umekuwa ukienezwa na mataifa ya Ulaya.

“Madini? Madini ya kufanya nini? Congo kutafuta madini!,” alisema Museveni akikanusha kuhusika na wizi wa hazina kubwa ya utajiri wa madini ya nchi hiyo jirani.

“Kuna madini mengi hata Uganda na mengi hayajachimbuliwa, kwa nini niende kuiba yale ya Congo? Kama hamjui jeolojia ya Afrika, madini yote yaliyo Congo yanapatikana pia Uganda na Tanzania, iweje niyaache madini kwangu niende kuyatafuta ya Congo?” amehoji Rais Museveni.

Baada ya Rwanda na Uganda kufanikiwa kumtoa Mobutu na kumweka madarakani Desiré Kabila na chama chake cha AFDL, haikupita miaka Kabila aliuawa mnamo Januari 16, 2001.

Baada ya kifo chake, nafasi yake ya urais ilichukuliwa na mtoto wake Joseph Kabila ambaye ndiye bado yupo madarakani nchini humo.

Weka maoni