Rais Museveni awataka raia watoe taarifa kuhusu polisi wala rushwa

195
Rais Museveni na watu wengine wakikata keki wakati wakisherehekea kitendo cha Mbunge Anywar kunusurika kifo

Rais wa Uganda amesema serikali yake iko tayari kuwachukulia hatua polisi wala rushwa, na kuwataka wananchi watoe taarifa kila waonapo polisi ambao hawana maadili.

Rais Kaguta Museveni amesema ukosefu wa usalama katika Wilaya ya Kitgum unasababishwa na maafisa wa usalama kujihusisha na mirungura.

“Tuliwaambia kwamba Serikali ya NRM italeta amani na amani ipo popote nchini. Hata hivyo, wahalifu wanawakosesha watu usalama, na ni kwa sababu takribani polisi wote ni wala rushwa,” amesema Museveni.

Rais Museveni ametoa kauli hiyo wilayani Kitgum wakati akiongea kwenye tafrija iliyoandaliwa na Mbunge wa FDC Beatrice Anywar baada ya kunusurika kifo katika ajali.

Mbunge Atim Anywar aliponea chupuchupu Machi, 2017, baada ya gari alilokuwemo akitokea msibani wilayani Lamwo kupinduka kutoka barabarani. Alipata majeraha na kuwahishwa hospitali.

Kwa mujibu wa Chimp Reports, Rais Museveni amesema “nina furaha kubwa sana kuungana na dada yangu, Beatrice Anywar, kusherehekea baada ya yeye kunusurika ajali tatu,”

Akiongea kuhusu mbunge huyo kutoka chama pinzani cha FDC, Rais Museveni amesema “huwezi kumuombea mabaya mtu kisa mmetofautiana kisiasa, badala yake unatakiwa umshawishi ajiunge na upande wako.”

Rais Museveni amewaambia raia waliokuwepo wakimtega sikio, kwamba chama chake cha NRM kina sera nyingi ikiwemo zile zihusuzo usalama, barabara, umeme, elimu, afya na maji, na kuwakumbusha viongozi kuhusu wajibu wao wa kuangalia ni wapi wamefikia katika utekelezaji wa sera hizo.

Weka maoni