Real Madrid yatwaa ubingwa wa Super Cup mbele ya Barcelona

152

Timu ya soka ya Real Madrid jana imeididimiza klabu ya Barcelona magoli 2 – Bila majibu katika Fainali ya Pili ya Super Cup. Ikumbukwe mchezo wa kwanza Real Madrid ilishinda 3 – 1 Mchezo ambao ulipelekea Crisitiano Ronaldo kufungiwa michezo mitano kwa kosa la kumsukuma mwamuzi na kosa la kedi nyekundu, Hivyo Real jana walicheza bila huduma yake.

Mchezo wa mkondo wa pili uliopigwa kwenye dimba la Santiago Bernabeu usiku wa kuamkia leo Real Madrid walianza kupata bao la kwanza kupitia kinda wa mabingwa hao wa Ulaya, Marco Asensio dakika ya 4 kabla ya mshambuliaji Karim Benzema kufunga goli la pili la ushindi mnamo dakika ya 39 kipindi cha kwanza na mpaka kipenga cha mwisho Real Madrid ikashinda 2 Barcelona 0.

Kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, Real Madrid waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini kwenye dimba la Camp Nou mwishoni mwa wiki kwa goli la kujifunga la Gerald Pique, Cristiano Ronaldo na Marco Asensio huku bao la kufutia machozi kwa upande wa Barcelona likifungwa na Lionel Messi kwa mkwaju wa penati.

Real Madrid wametwaa ubingwa huo kwa jumla ya goli 5-1 dhidi ya Barcelona na kumfanya kocha Zinedine Zidane kuongeza idadi ya vikombe na kuweka rekodi ya kuwa kocha mwenye mataji mengi (7) kwa muda mfupi klabuni hapo .

 

Weka maoni