Ripoti za Warundi elfu 10 kukimbilia Rwanda mwezi huu ni uongo – UNHCR

353
Mtoto akiwasha moto katika kambi ya wakimbizi wa kirundi ya Mahama iliyoko wilayani Kirehe Mashariki mwa Rwanda (Picha/New Times)

Shirika la kimataifa la kuhudumia wakimbizi la UNHCR limezikanusha ripoti za Warundi zaidi ya elfu kumi kukimbilia Rwanda mnamo Aprili 2017 na kuwataka waliozisikia wasizisadiki.

Shirika hili limesema idadi halisi ya Warundi hao ni 406 na ni ndogo ikilinganishwa na miezi iliyotangulia ya Machi (595), Februari (791) na Januari (732).

Kwa ujumla Warundi walioingia Rwanda kutafuta kimbilio la hifadhi mwaka huu ni 2,524, ambapo kwa ujumla Rwanda imewapokea wakimbizi hao 94.581 tangu Aprili 2015.

UNHCR imesema watu 9,236 kati ya hao 94.581 si wakimbizi tena kwani baadhi walirudi makwao huku wengine wakikosekana kuchukua posho katika kambi ya Wakimbizi ya Mahama.

Hii kimuktasari inamaanisha kuwa wakimbizi wa Kirundi walio nchini Rwanda mpaka leo ni 85,345, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UNHCR kwa vyombo vya habari.

Burundi imekuwa ikitikiswa na misukosuko yenye misukumo ya kisiasa tangu Aprili 2014 wakati Rais Pierre Nkurunziza alipothibitishwa kama mgombea urais kwa awamu ya tatu.

Maelfu ya watu hasa wale walioegemea upande wa upinzani walilazimika kuyakimbia makazi wakiwataja vijana wa chama tawala wa Imbonerakure kuwa wanawatishia maisha yao.

Kwa nyakati tofauti Burundi iliituhumu Rwanda kwa kuwadhamini waasi wanaolenga kuipindua serikali ya Nkurunziza, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha ikisema hayana unyayo wala utosi.

Weka maoni