Rwanda kupata walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania

741
Rais Kagame (kulia) na Rais Magufuli (kushoto) katika hafla iliyofanyika Kigali Serena Hotel mwaka jana wakati Magufuli akiwa ziarani nchini Rwanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli, ameahidi kuipa Serikali ya Rwanda msaada wa walimu wa kufundisha Kiswahili.

Waziri wa Elimu wa Rwanda, Dr Papias Musafiri, kwa niaba ya Rais Kagame, amewasilisha kwa Rais Magufuli ombi la kutaka kupewa walimu wa kufundisha lugha hiyo nchini Rwanda.

Rais Dkt John Pombe Magufuli, amepokea ujumbe toka kwa Rais Kagame wa Rwanda, Ikulu jijini Dar es Salaam (Picha/Bongo5)

Rais Magufuli amepokea ombi hilo kwa mikono miwili na kuipongeza Rwanda kwa kuamua Kiswahili kifundishwe katika shule nchini Rwandakwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari.

Pamoja na Waziri Musafiri kuwasilisha barua hiyo ya Rais Kagame, Rais Magufuli na Dkt Musafiri wamezungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda ikiwemo katika sekta ya elimu hususan maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Aidha Rais Magufuli ameipongeza Rwanda kwa kuamua lugha ya Kiswahili ianze kufundishwa katika shule zake na ameahidi kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kuja kufundisha lugha hiyo, kwa mujibu wa tangazo kutoka ikulu kwa vyombo vya habari.

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Dkt. Musafiri Papias, Waziri wa Elimu wa Rwanda na Mjumbe maalumu wa Rais Paul Kagame alipokutana naye Ikulu jijini Dar es salaam, Wengine ni Balozi wa Rwanda nchini Mhe. Eugene Kayihura na Afisa Mwandamizi wa Ubalozi Bw. Issa Mugabutsinze. (Picha/Bongo5)

Akielezea mswada wa marekebisho ya Sheria ya Lugha Rasmi bungeni, Waziri wa Michezo na Utamaduni, Bi Julienne Uwacu, alisema urasimishwaji wa Kiswahili utawanufaisha raia wengi hasa wafanyabiashara.

Alisema zipo nafasi nyingi za uwekezaji katika eneo la Afrika Mashariki, na Kiswahili ni moja kati ya vyombo muhimu ambavyo Wanyarwanda wanatakiwa wavichangamkie kwa manufaa yao.

Haijajulikana kama Rwanda inahitaji walimu wangapi kutoka Tanzania, na wala haijawekwa bayana kama Wanyarwanda waliojifunza Kiswahili watafikiriwa katika utoaji wa ajira kwa walimu wa Kiswahili.

Rwanda ilipata uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki miaka 10 iliyopita.

Miaka ya nyuma Rwanda iliwaajiri walimu kibao wa Kiingereza kutoka hasa Uganda na Kenya baada ya kujihakikishia uanachama wa Jumuiya ya Mataifa yanayotumia Kiingereza ya Common Wealth.

Wazo moja

  1. Mbona ni shida kubwa kuwaleta walimu kutoka Tanzania wakati tuna wanyarwanda wa kutosha na wajua Kiswahili zaidi ya sana? Mini sikubaliani kamwe na hoja hilo kwani kuna waswahili wenzangu ambao mpaka sasa hawajapata kazi. Huenda ikawa kama vile walivyowaleta walimu wa kimombo kutoka Uganda ila mavuno yalikuwa bure. Ikiwa Rwanda inapromoti made in Rwanda, kwanini hawaanzii kwa wanyarwanda werevu ambao wameshapevuka katika lugha ya kiswahili? Mimi ni tayari kutoa mchango wangu

Weka maoni