Rwanda kuwapa hifadhi wahajiri wanaouzwa kiutumwa Libya

334
Wahamiaji hukusanywa pamoja na watekaji wao wakati wakisubiri kununuliwa kwenye soko la utumwa nchini Libya

Waziri wa nchi za nje wa Rwanda ambaye pia ndiye msemaji wa serikali, Bi Louise Mushikiwabo, amesema Rwanda imekerwa na utumwa unaoendelea dhidi wa wahamiaji nchini Libya.

Amesema ingawa Rwanda ni nchi ndogo, lakini haiwezi kushindwa kuwapokea na kuwakarimu Waafrika ambao wanaendelea kuuzwa kiutumwa nchini Libya.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Bi Mushikiwabo amesema Wanyarwanda wamepitia historia mbaya ya kuishi ukimbizini miaka mingi na bila utaifa, na hiyo ndiyo inayowafanya wawe na moyo wa kuwafadhili watu walio katika hali ya dhiki.

Ikumbukwe kuwa mnamo mwaka 1994 Rwanda ilikumbwa na mauaji ya kimbari yaliyotekelezwa dhidi ya jamii ya Watutsi na kugharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja.

Mauaji hayo yalisimamishwa na majeshi ya RPF-Inkotanyi ambayo yaliivamia nchi hiyo ya Afrika ya Kati kutoka Uganda, ambapo lengo la uvamizi ilikuwa ni kuikomboa Rwanda.

Waziri wa nchi za nje wa Rwanda Bi Louise Mushikiwabo

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Musa Faki Mahamat ameishukuru Rwanda kwa kuamua kuwasaidia Waafrika ambao wanataabika nchini Libya.

Amesema Rwanda imemuambia siyo tu kuwapa hifadhi wahamiaji husika, bali itagharamia hata usafirishwaji wao kutoka Libya hadi Rwanda.

Mahamat amesema Rwanda imesema watakaoamua kurudi makwao itawawezesha kufika nchini mwao.

Waafrika kutoka Gambia, Niger na Senegal wamekuwa wakiripotiwa kutekwa nyara nchini Libya wakielekea Ulaya kupitia Bahari ya Mediteranea.

Shirika la kuwahudumia wahamiaji duniani International Organization for Migration (IOM) limesema bado wahamiaji wanaendelea kuuzwa katika soko la utumwa nchini Libya.

Wanaolengwa na utumwa huo imeripotiwa ni Waafrika waishio kusini mwa jangwa la Sahara.

Mwandishi wa CNN ambaye amechunguza kwa kina biashara hiyo haramu, amesema mtu mmoja huuzwa dola 400 kufikia 500 kulingana na uwezo wake wa kufanya kazi.

Watumwa hao hulazimishwa kuwapigia simu familia zao ili walete hela ya kukombolewa.

Ripoti zinasema wahamiaji huingizwa na watekaji wao katika nyumba za kuhifadhi bidhaa wakiwa wamejazana wakati wakisubiri kuingizwa kwenye soko la utumwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mataifa, Alpha Condé ameitaka Serikali ya Libya ichunguze vitendo hivyo vya utumwa ambavyo vimekithiri na kuwafungulia mashtaka wale wote wanaohusika.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imesema imeanza kuchunguza magendo hiyo ya binadamu, na kuahidi kuwafikisha wahusika mbele ya vyombo vya sheria.

Libya imekuwa nchi ya machafuko ya kisiasa hasa baada ya Kanali Mouamar Gadhafi kupinduliwa na majeshi ya kujihami ya NATO mwaka 2011.

Weka maoni