Rwanda: NEC yakinzana na wagombea urais watarajiwa ukusanywaji wa misaada

203
Philippe Mpayimana

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Rwanda (NEC) imeawaonya ambao wameshajitangaza kuwa watawania urais kuwa muda wa kujinadi na kukusanya misaada kutoka kwa raia haujawadia.

Vipo vyama ambavyo vimetoa taarifa kwa umma vikitaka kuwepo ukusanywaji wa pesa zitakazotumika kuendesha kampeni. Uchaguzi mkuu utafanyika mnamo Agosti, 2017.

NEC imesema mienendo ya wanasiasa hao imekiuka sheria kwani wagombea hawajathibitishwa, ikisema wanaojiita wagombea waache kukurupuka.

Katibu Mtendaji wa NEC, Bwana Munyaneza Charles, amesema “wagombea hawajaidhinishwa, tutaanza kupokea maombi yao ya kugombea kuanzia tarehe 12 hadi 23 Juni, na watakaoruhusiwa kugombea watatangazwa tarehe 7 Julai.”

“Kwa hiyo mpaka leo hakuna mgombea, ukusanywaji huo wa misaada siyo halali na hata kama ungekuwa halali wangefanya hivyo kwa mujibu wa sheria,” ameongeza.

Aidha Bw Munyaneza amesema sheria inatoa muongozo kuhusu njia za wanachama au hata chama chenyewe kukusanya misaada kwa ajili ya mgombea, na siyo kama wanasiasa hawa wanavyoendesha shughuli zao, kwa mujibu wa Igihe.

Frank Habineza ambaye ni mwasisi wa Chama cha upinzani cha Green Party ambaye kimemtangaza kuwa ndiye atagombea kwa tiketi yake, amewataka wanachama wakusanye faranga biliyoni moja na nusu zitakazotumika katika mbio za urais.

“Ambao mna mashamba uzeni, uzeni mahindi, uzeni viazi ili kuwezekanisha uchaguzi. Changia kadri ya uwezo wako kwani uungaji mkono wenu unahitajika. Ni budi kila mwanachama ajitolee ili tuweze kushinda uchaguzi,” alisema Bw Habineza, mnamo Machi 2017, akiwahutubia wanachama wa Green Party.

Katibu Mkuu wa Green Party, Jean Claude Ntezimana, ameliambia Habari Pevu kuwa haoni kama kuna tatizo kukusanya misaada ya kuendeshea kampeni kwani sheria inaruhusu.

Amesema ingawaje NEC haijaidhinisha wagombea, lakini wagombea hao kwanza hupitishwa na vyama vyao na ndiyo maana Frank Habineza akawatolea mwito wanachama kuchangisha pesa kwani chama kilikuwa kimesha muidhinisha.

“Hatujaanza kukusanya hiyo misaada ila hata tungekuwa tumeanza sioni cha kutulaumu, wanachama ndio waliambiwa wajiandae na uchaguzi na sheria inaruhusu wanachama kukusanya pesa kwa ajili ya mgombea wao,” amesema Bw Ntezimana katika mahojiano na Habari Pevu.

Mpayimana Philippe ambaye alisema atawania urais kama mgombea huru, aliwataka raia wampe pesa kama wanavyotoa sadaka makanisani au wanavyozisaidia timu zao pendwa.

Mpayimana alisema ameshamteua mtu atakayepokea fedha hizo ambapo ametoa hata akaunti ya benki na namba ya simu ambavyo watu wanaweza wakatumia kuwasilisha udhamini wao.

Ifahamike kuwa ni haramu kampeni za mgombea kudhaminiwa na watu kutoka nje ya nchi, dini na asasi zozote zile, ziwe za kiserikali au za kibinafsi.

Ikumbukwe kuwa miaka miwili iliyopita Katiba ya Jamhuri ya Rwanda ilifanyiwa marekebisho kuhalalisha Rais Paul Kagame kugombea urais kwa awami ya tatu mfululizo.

Kwa mujibu wa kifungu namba 101 ambacho kimerekebishwa, Rais Kagame anayo haki ya kuwania urais mara tatu zingine, ambapo anaweza kukalia kiti cha urais hadi mwaka 2034.

Weka maoni