Rwanda ni nyumbani, nimekuja kuwatembelea ndugu zangu – Yvonne Chaka Chaka

516
Yvonne Chaka Chaka leo hii akiwa Jijini Kigali

Nguli wa muziki wa Afrika Kusini Yvonne Chaka Chaka maarufu kama Princess of Africa (Malkia wa Afrika) amewasili Jijini Kigali kwa ajili ya mkutano wa Shirika la Global Fund.

Muda mfupi baada ya kutinga jijini hapa, Chaka Chaka amesema akija Rwanda anajihisi kama mtoto mwenda kwao.

“Nimekuja nyumbani, Rwanda naichukulia kama maskani yangu ya pili, nimekuja kuwatembelea ndugu zangu niwajulie hali,” amenukuliwa na Igihe.

Yvonne Chaka Chaka akiwa na mwandishi wa Igihe Murungi Sabin ambaye ndiye wamefanya mahojiano

Akizungumzia kipaji chake cha muziki, amesema asingekuwa na uwezo wa kuimba asingepata dili la Global Fund ambapo ni balozi wa shirika hili linalojishughulisha na masuala ya afya.

“Nisingekuwa msanii mzuri nisingekuwa nafanya kazi na Global Fund au UNICEF (Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto) na mashirika mengine,” amesema Chaka Chaka.

“Nimeona malaria inavyowaua watu, nimeona maisha ya Waafrika yalivyo magumu ndipo nikaamua kutumia kipaji changu kushirikiana na marais kuboresha maisha ya raia,” ameongeza.

Katika hatua nyingine msanii huyu amesema mwezi ujao atazindua santuri yake ya ishirini na tatu ambayo mtoto wake alimsaidia kutengeneza.

Amesema kuna wimbo alioshirikiana na Ali Kiba ambao haujatoka na kuwataka mashabiki wake wakae mkao wa kula, na kuongeza kuwa kuna wimbo mwingine anajipanga kumshirikisha Lady Jay Dee.

“Mwishoni mwa mwaka jana nilikuwa Ghana, wiki nne zilizopita nilikuwa Zimbabwe, muda kidogo kabla ya hapo nilitumbuiza Washington, Uingereza na kwingineko, nimeimba nyimbo zangu mpya. Kinachofuata sasa ni kuwasaidia wasanii wanaochipukia, nimefanya kazi na Ali Kiba wimbo utatoka hivi karibuni, najipanga kufanya kazi na Lady Jay Dee kutoka Tanzania,” amesema Yvonne Chaka Chaka.

Chaka Chaka amekuja na mdhamini wake (kulia)

Mwaka 2011 Chaka Chaka alikuja Rwanda ambapo, akishirikiana na Mke wa Rais wa Rwanda Jeannette Kagame, waliwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililoukumba Mkoa wa Kaskazini.

Mwaka 2007 pia alikuwa Rwanda alipofanya tamasha la kihistoria Jijini Kigali. Aliwaacha hoi mashabiki wake katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuundwa kwa Mji wa Kigali.

Shirika la Global Fund ni mshiriki mkubwa wa Rwanda katika sekta ya afya ambapo limekuwa likidhamini shughuli za kupambana na ukimwi, malaria na kifua kikuu.

Kikao cha kamati tendaji ya shirika hili kinatarajiwa kufanyika mjini Kigali kesho na keshokutwa na kitakutanisha wadau wanaokadiriwa kuwa 250 akiwemo Chaka Chaka.

Global Fund leo wameitembelea Dispensari ya Gikondo iliyoko wilayani Kicukiro ambayo wanaidhamini, kabla ya kuitaja Rwanda kuwa ni mfano mzuri wa nchi zitumiazo misaada ya wafadhili ipasavyo.

Yvonne Chaka Chaka amesema hatua ambayo Rwanda imepiga kuimarisha sekta ya afya ni ya kupigiwa makofi.

Chaka Chaka akiongea na msimamizi wa kazi zake, Marriot Hotel

Yvonne Chaka Chaka, 52, anatunga na kuimba nyimbo, lakini pia ni mjarisiamali na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini. Ni msanii anayeheshimika nchini humo tangu mwaka 1990.

Album yake ya kwanza inaitwa ‘I’m in Love With a DJ’. Nyimbo kama ‘I’m burning up’, “I Cry for Freedom”, “Umqombothi” ni miongoni mwa zile zilizomzolea umaarufu wa kimataifa.

Weka maoni