Rwanda yaadhimisha sikukuu ya ukombozi kwa mara ya 23

246
Wananchi wakipunga vibendera kumkaribisha Rais Kagame. Picha/Urugwiro Village.

Leo Wanyarwanda wamesherehekea sikukuu ya ukombozi kwa mara ya 23 tangu majeshi ya kikosi kilichokuwa kinaongozwa na Rais Kagame kijihakikishie udhibiti wa nchi mwaka 1994.

Kukombolewa kwa Rwanda kuliambatana na kusimamisha mauaji ya kimbari yaliyokuwa yanafanywa dhidi ya Watutsi kwa usimamizi wa serikali iliyokuwepo madarakani.

Leo Rais Paul Kagame amejiunga na wakazi wa Wilaya ya Nyabihu, Jimbo la Magharibi, ambapo aliwakumbusha juhudi zilizofanyika kuikomboa Rwanda kwa mtutu wa bunduki.

Rais Kagame ameuambia umati wa waadhimishaji kuwa idadi kubwa ya Wanyarwanda walizaliwa baada ya mwaka 1994, na wao ndio nguzo na matarajio kwa taifa la kesho.

Kabla ya kuongea na wananchi, Rais Kagame na mkewe Jeannette Kagame wamekagua hospitali ya wilaya ya Shyira inayotarajiwa kuwanufaisha raia wapatao laki mbili waishio maeneo jirani.

Rais Kagame na mkewe pia walitembelea nyumba zilizojengwa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) kwa ajili ya kaya 108 zisizojiweza, kama sehemu ya juhuzi za kuendelea kujikomboa kiuchumi.

“Wanyarwanda walio wengi walikuwa hawajazaliwa mwaka 1994, ni vijana watakaokuwa na mustakbali mzuri,” amesema Rais Kagame ambaye yupo madarakani tangu mwaka 2000.

“Kujikomboa ni kuondokana na uongozi mbaya na madhara yake ikiwemo njaa, umaskini na mizozo. Tumeshaupiga chini uongozi mbaya leo tunapambana na madhara yake,” ameongeza.

Rais Kagame ambaye kwa nyakati tofauti aliwahamasisha Wanyarwanda kufanya juu chini kuhakikisha wanaondokana na utegemezi wa misaada ya wafadhili, safari hii amesema,

“Ukiwategemea wengine katika maisha, wao ndio wataamua kama unastahili kuishi au kufariki dunia. Tunatambua uwezo wetu kwani tunajua tulivyotoka mbali.”

“Tuna uwezo wa kuliendeleza taifa letu, tuna uwezo wa kupata maendeleo kama yale yanayoshuhudiwa katika nchi zingine duniani,” amesisitiza Rais Kagame.

Aidha, Rais wa ‘nchi ya milima elfu moja’ amewataka wananchi kushiriki juhudi za kulinda usalama: “Tuendelee kutunza usalama kwa kuwa ndio ulituwezesha kupata maendeleo.”

Rais Kagame akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Nyabihu leo hii. Picha/Urugwiro Village.

Rwanda ni nchi iliyoshuhudia machafuko ya kikabila tangu mwaka 1959 ambayo yaliendelea hafi kufikia mwaka 1994 yalipotekelezwa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi.

Mauaji husika yaligharimu maisha ya watu wanaokadiriwa kuwa ni miliyoni moja na elfu 74, kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Rwanda zilizotokana na utafiti wa mwaka 2002.

Serikali ya Rwanda haithamini tarehe 1 Julai 1962 ambapo taifa hilo lilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mbeljiji kisa mauaji yaliendelea hata baada ya uhuru kupatikana.

Juzijuzi Waziri wa Sheria Johnston Busingye, alisema Rwanda haiadhimishi uhuru kwa kuwa mwaka 1962 ni mwaka ambao Rwanda ilishuka kwenda kuzimu.

Serikali ya Rais Gregoire Kayibanda (1962-1973) na ile ya Rais Juvénal Habyarimana (1973-1794), zinakosolewa kwa kuwabagua Watutsi na kuchochea mauaji dhidi yao.

Rais Kagame aliyeongoza majeshi yaliyosimamisha mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyofanyika Aprili-Julai 1994, anatarajiwa kushinda uchaguzi mkuu wa Agosti 2017.

Weka maoni