Rwanda yasitisha ushirikiano wake na Human Rights Watch

415
Johnston wa Sheria wa Rwanda Johnston Busingye (Picha/Umuseke)

Serikali ya Rwanda imechukua uamuzi wa kusitisha ushirikiano wake na Shirika la kimataifa la kupigania haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW).

Waziri wa Sheria Johnston Busingye ambaye ndiye Mwanasheria Mkuu pia, amesema hatua hiyo imepigwa kufuatia shirika hilo kutoa ripoti zinazokinzana na maslahi ya Wanyarwanda.

“Tumeona ushirikiano wetu na HRW hautoi matunda, hauna tija, tumeona bora tuwaache waendelee kuandika wanavyotaka,” Busingye amewaambia waandishi wa habari mjini Kigali.

“Hatuna kalamu zao, hatuna karatasi zao, ambacho tumeamua kuepuka ni kujibizana nao, hatutaki mawasilano nao,” ameongeza Waziri Busingye, hapo jana Jumanne.

Aidha Bw Busingye amesema ingawaje HRW wanajiita wapigania haki, lakini ripoti zao zinapotosha ukweli, hivyo kupelekea serikali kuvunja uhusiano uliokuwepo baina yao.

Amesema anachojua tu ni kwamba HRW ni asasi ambayo si ya kiserikali, na kuongeza kuwa wanaoichukulia kama shirika la wapigania haki wanakosea sana.

Tangu iundwe mwaka 1988, HRW imekuwa ikiendeshwa kwa misukumo ya kisiasa na hata haistahili kuitwa shirika la kimataifa kwani haisaidii kuleta maendeleo, Busingye ameongeza.

Shirika hili limetoa ripoti kedekede likiishutumu serikali ya Rwanda kuwakandamiza raia wa kawaida na wanasiasa wanaothubutu kuikosoa, madai ambayo serikali imeyatupilia mbali.

Ilipofika mwaka 2011, pande mbili zilikubaliana kwamba Rwanda itakuwa inapewa nafasi ya kujitetea dhidi ya shutuma zilizomo kwenye ripoti kila kabla ya ripoti kutoka.

Mnamo Aprili 2014, Waziri Busingye alikutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa HRW barani Afrika, Lewis Mudge, na kumuelezea jinsi HRW ilivyokiuka makubaliano hayo.

Kwa nyakati tofauti, HRW iliituhumu Rwanda kwa kuwadhamini waasi wa M23 wa huko DR-Congo, kuminya uhuru wa vyombo vya habari na kuwanyanyasa wapinzani wake.

Mwaka jana HRW walitoa ripoti kuhusu walichokitaja kuwa ni ukandamizaji uliokithiri kwenye kituo cha tiba na marekebisho ya tabia kwa watumiaji wa dawa za kulevya, wazururaji na wamachinga kilichoko Gikondo mjini Kigali, kijulikanacho kwa jina maarufu kama “Kwa Kabuga”.

Serikali ya Rwanda ilisema ripoti hiyo imesheheni uongo tu na kuwataka raia waipuuzie.

Wazo moja

  1. Hata hivyo Rwanda ilikuwa imechelewa kuachana nao, sijaona ripoti yao ambayo hawajatia chumvi. Wanaweza wakaongea kitu ambacho kipo ila watakiongezea nyama mpaka wanaonekana matahira. Kwa hiyo sioni kama kuna ambacho tutapungukiwa kwa kusitisha ushirikiano nao. Big up kwa waziri wetu Busingye.

Weka maoni