Rwanda yawapata vifaru 10 weusi kutoka Afrika Kusini

1324
Harambee ya kuwapeleka vifaru kwenye gari

Bodi ya Maendeleo nchini Rwanda (RDB) imetoa taarifa ya Rwanda kuwapata vifaru 10 weusi kutoka Afrika Kusini, ikiwa ni baada ya miaka 10 vifaru kutoweka nchini humo.

Miaka ya sabini Mbuga ya Wanyama ya Akagera iliyoko Mashariki mwa Rwanda ilikuwa ni hifadhi ya vifaru wapatao hamsini lakini majangili waliwaua hadi kuwamaliza mwaka 2007.

Vifaru hao kutoka Afrika Kusini wamefikishwa Rwanda salama salimini wakiwa buheri wa afya baada ya kusafirishwa umbali wa kilomita elfu nne, uongozi wa Hifadhi ya Akagera umesema.

Kifaru ndiye mnyamapori wa pili kwa ukubwa baada ya tembo. Huyu anayevutwa ni miongoni mwa walioletwa Rwanda.
Kifaru akiingizwa kwenye gari

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Clare Akamanzi, amesema ujio wa vifaru hao umefungua ukurasa mpya katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

“Tunawashukuru wadau wote waliofanikisha shughuli hii, tumejiandaa vya kutosha kuwapokea (vifaru hao) na kuwahakikishia usalama ili kukuza sekta ya utalii na kuwanufaisha raia kwa ujumla” amesema Akamanzi.

Rwanda inatarajia kuwapata vifaru wengine kumi kutoka Afrika Kusini katika siku za mbeleni.

Ni mradi unaoendeshwa kwa ushirikiano wa shirika lisilo la kiserikali la Akagera Parks linalotunza Hifadhi ya Akagera na udhamini wa mfanyabiashara mashuhuri kutoka Marekani Howard G. Buffett na Serikali ya Uholanzi.

“Miaka mingi iliyopita, tukiendelea kupiga vita uwindaji haramu wa vifaru barani Afrika, nilimuahidi Rais Kagame kuwa nitatoa mchango wangu kurejesha vifaru nchini Rwanda kwani nina imani nchi hiyo itawatunza vizuri,” amesema Howard G. Buffett.

Vifaru popote walipo duniani wanakabiliwa na tisho la kuwindwa kiharamu.

Soko la pembe za wanyamapori hao ni kubwa hasa barani Asia kwani hutumiwa kama dawa.

Mwaka 2012 mahakama nchini Afrika Kusini ilimhukumu kifungo cha miaka arobaini raia mmoja wa Thailand aliyepatikana na hatia ya kuuza pembe za vifaru.

Mwaka huo zaidi ya vifaru miatano waliuawa nchini humo na wawindaji haramu.

Wazo moja

Weka maoni