Sababu za Rwanda kupaisha tozo la kuingia mbuga ya sokwe hizi hapa

465
Sekta ya utalii wa sokwe wa milimani ndiyo ya kwanza kuingizia Rwanda fedha za kigeni

Sokwe ni wanyama wanaokabiliwa na hatari ya kutoweka duniani, na hiyo ni moja kati ya sababu za Rwanda kuimarisha usalama wao kwa ajili ya vizazi vijavyo, RDB imesema.

Majuzi RDB (Bodi ya Maendeleo Rwanda) ilitangaza kupandishwa gharama ya kuwatembelea wanyamapori hao toka dola 750 hadi dola 1500, uamuzi uliozua gumzo mitandaoni.

Mtangazaji wa televisheni ya CNBC Africa, Georgie Ndirangu, ni miongoni mwa wale waliokemea hatua hiyo ya serikali ya Rwanda, akisema haimuingii akilini. Bonyeza hapa kuangalia malalamiko yake.

Amesema ni dhahiri kuwa ongezeko la tozo la kuingia hifadhini litasababisha watalii kupungua kwani sokwe wa Uganda na wale wa Kongo wanatembelewa kwa tozo nafuu (dola 400 kwa wale wa Congo na 600 kwa wale wa Uganda).

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo Rwanda (RDB), Clare Akamanzi, amesema uamuzi huo haujakurupukiwa na uliidhinishwa baada ya kuungwa mkono na wadau mbalimbali.

Amesema kupungua kwa idadi ya watalii kutasaidia kupunguza athari za muingiliano baina ya watalii na wanyamapori hao, ambapo wengine huwajeruhi na kuwasababishia vifo.

“Kwa hiyo tunatakiwa tuchukue hatua za kupunguza wingi wa watu na tuendelee kuwalinda wanyama hao kwa ajili ya vizazi vijavyo,” Clare Akamanzi ameiambia Habari Pevu.

Aidha, Akamanzi amegusia mkakati wa serikali wa kuongeza kanda zilizozuiliwa kati ya hifadhi ya sokwe na makazi ya wananchi, ili kuongeza usalama endelevu wa wanyamapori hao.

Clare Akamanzi, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Maendeleo nchini Rwanda

Wiki moja tu baada ya kutangazwa kwa tozo mpya, watalii 25 walijitokeza na kulipa gharama hiyo, kwa mujibu wa Akamanzi.

Sekta ya utalii wa sokwe wa milimani ndiyo ya kwanza kuingizia Rwanda fedha za kigeni.

Ughali wa kuingia mbugani unatarajiwa kunufaisha hifadhi zingine na raia waishio karibu na mbuga za wanyama, ambapo kwa kawaida serikali huwatengea asilimia 5 ya pato la utalii.

Kutokana na sera hiyo iliyopo kuanzia mwaka 2005, serikali kufikia sasa imetoa faranga biliyoni 2,8 kama udhamini kwa miradi 600 katika tarafa 45 zinazokaribiana na mbuga za wanyamapori.

Miradi hiyo ni pamoja na ile ya ujenzi wa shule na ule wa vituo vya afya, usambazaji wa umeme vijijini, viwanda vya kusindika maziwa, ufugaji wa kisasa wa nyuki na mingineyo mingi.

Akamanzi amesema kuanzia mwakani serikali itatenga asilimia 10 kama ufadhili kwa miradi ya miundoimbinu katika maeneo yapakanayo na hifadhi za wanyama.

Hifadhi ya Volkeno iliyoko Kaskazini mwa Rwanda, ndiyo hifadhi pekee ya sokwe nchini humu na ni nyumbani kwa sokwe wa milimani wapatao 300.

Weka maoni