Sanjay Dutt kuifaidi Tanzania siku 21

312
Sanjay Dutt, muigizaji mkongwe wa filamu za kihindi

Muigizaji mkongwe na  anayefanya vizuri kwenye soko la filamu India, Sanjay Balraj Dutt, aliyekuja Tanzania kwa ajili ya mapumziko anatarajiwa kudumu kwa siku 21 ambapo atatembelea mbuga za wanyama na vivutio mbali mbali vilivyopo nchini humo.

Ujio wa Sanjay Dutt umethibitishwa na mwenyeji wake ambaye ni Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali ambaye amesema uwepo wa msanii huyo ni kipimo cha kuwa sekta ya utalii nchini inaendelea kupanuka.

“Uwepo wa Sanjay Dutt nchini ni fursa kubwa sana. Wahusika wa utalii hapa nchini wakiona fursa katika kuutangaza zaidi utalii wetu ni vyema pia wakamtumia kwani mtu huyu ni mkubwa sana kwenye sanaa ya filamu. Lakini pia kuja kwake hapa nchini ni wazi tunazidi kukua kwenye sekta hii, na tutapata mapato kupitia kuwepo kwake kwani atakuwepo kwa takribani siku 21” alisema Mhe. Gulamali

Hata hivyo mbunge huyo amewataka waigizaji wa filamu nchini kuchangamkia fursa ya kukutana na muigizaji huyo kwa ajili ya kupata madini yatakayowasaidia kukuza na kupanua soko la filamu, kwa mujibu wa EATV.

Muigizaji Sanjay Dutt (kushoto) akipeana mkono na Mbunge Gulamali

“Huyu ni muigizaji mkubwa ningewashauri wasanii wa nyumbani wasimuachie akaondoka hivihivi.  Kama uongozi wa wassnii wa filamu wataona fursa kwake wasisite kunitafuta ili niweze kuwakutanisha naye kwani haitashindikana kutenga siku moja kwa ajili ya  mazungumzo ambayo yatakuwa na faida kwenye sanaa ya nyumbani lakini kama wakiona hakuna haja basi hakuna shida kwani wao walio kwenye field ya uigizaji ndiyo wanaojua kitu gani wanataka”, aliongeza.

Sanjay Dutt amefika Arusha mapema leo akitokea Dar es salaam kwa ajili ya kuzuru mbuga za wanyama, Ngorongoro, Serengeti, mbuga ya Selou na vivutio vingine vilivyopo nchini Tanzania.

Angalia moja kati ya filamu alizoziigiza Sanjay Dutt inayoitwa Vaastav ambayo ilitoka mwaka 1999.

Sanjay Dutt ambaye alizaliwa mwaka 1959, alianza kuigiza akiwa na umri wa miaka 22 na kufikia leo ameigiza filamu 100.

 

Weka maoni