Senderi atoa video ya kumnadi Rais Kagame na chama tawala

641
Rais Kagame na Bazivamo Christopher kutoka chama tawala, kwenye wimbo mpya wa Senderi International Hit

Video ya wimbo wa ‘Komeza utuyobore’ (endelea kutuongoza, kwa Kiswahili) wa msanii Senderi International Hit imeshatoka. Anamsifia Rais Kagame na chama chake cha RPF-Inkotanyi.

“Nimeona wananchi walio wengi wanapenda uongozi wake na alipowafikisha, nimekwenda vijijini nikajionea wanamuita ‘mzee kijana’, ‘mzee wa kwetu’ ikanipa wazo la kutengenezaz huu wimbo kwa ajili yao,” amesema msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Eric Nzaramba.

Video imesheheni picha nyingi hasa zile za Rais Kagame akiwa amewatembelea wananchi wa vijijini, na zile za majengo ikiwemo Kigali Convention Centre ambayo ndiyo inaongoza kwa ughali barani Afrika.

Baadhi ya sehemu za KIgali Convention Centre, majengo ya kifahari yanayopatikana katika Tarafa ya Kimihurura, Wilaya ya Gasabo, Jijini Kigali

Zimo pia picha za ng’ombe waliotolewa kupitia mradi wa Girinka Munyarwanda (Miliki ng’ombe Mnyarwanda) ulioanzishwa na Rais Kagame, unaolenga kuwatoa wananchi wasiojiweza katika lindi la umaskini, ambapo kila kaya hupewa ng’ombe.

“Wananchi hawatasahau Kagame alivyowapa ng’ombe leo wanakunywa maziwa, na mtu ambaye amekupa maziwa huwezi kumkataa, lazima utampenda,” ameongeza Senderi katika mahojiano na Habari Pevu.

Msanii huyo wa ngoma za miondoko ya Afrobeat, amesema mbali na wanavyoviongea wananchi, hata yeye kama yeye ana vitu vingi anavyomkubali Rais Kagame ikiwemo sera zake za mahusiano ya kimataifa.

“Napenda anavyoshirikiana na nchi za nje, watu walikuwa wanaijua Rwanda kwa genocide lakini leo wanaijua Rwanda kwa uongozi mzuri, sekta ya ICT imeendelea, majeshi yetu hupelekwa nchi zingine katika operesheni za kurejesha amani, kwa mfano Darfur, Central African Republic, wanajeshi wetu wanapigania amani na upendo.”

“Hata mimi alinipa tiketi ya ndege ya kwenda kutembea Mexico, nimeshukuru kabisa, nikasema ng’oja nimtungie wimbo aone kama mimi siyo mnafiki, na siyo mimi tu kila Mnyarwanda ana kitu ambacho amemfanyia,” ameongeza.

Alipoulizwa jinsi Rais Kagame atakavyojua kuwa kuna wimbo ameimbiwa, haya ndiyo majibu yake: “Najua anapenda wasanii, anapenda kusoma mnavyoandika nyinyi waandishi wa habari, mkiandika najua atasoma.”

Kwa mtazamo wa Senderi, Rais Kagame anafaa kuendelea kuongoza Rwanda mpaka mwaka 2024. Hapo atakuwa ameifikisha Rwanda kuzuri na atakuwa anatakiwa aondoke mamlakani ili aweze kuishughulikia familia yake ipasavyo, kwa mujibu wa maelezo ya msanii huyo.

“Mwaka 2024 naweza kumuombea aondoke madarakani kwani na familia yake inamtaka, ndio ushauri wangu.”

Rais Kagame siku za nyuma alitangaza kutokuwa na nia ya kuendelea kuongoza Rwanda baada ya mwaka 2024, akisema ni vyema Wanyarwanda wakaanza kufikiria kuhusu atakayefaa kuchukua nafasi yake.

Mwaka 2015 katiba ya Rwanda ilirekenbishwa na kumruhusu Rais Kagame aongoze Rwanda mpaka mwaka 2034 endapo raia wataendelea kumpigia kura.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu, ambapo orodha ya wale ambao wameshatangaza kuwa na nia ya kushindana naye imeshakuwa ndefu.

Aidha Senderi amewataka mashabiki wake wakae mkao wa kula kwani video ya wimbo wake wa Convention aliomshirikisha Bruce Melody itatoka katika siku za hivi karibuni.

Weka maoni