Serikali ya Rwanda kuwanyang’anya vyeti makandarasi wasiowalipa vibarua

363
Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Watumishi wa Umma na Ajira, Bw Gaspard Musonera

Huku idadi ya makandarasi wasiowalipa vibarua wao ikizidi kuongezeka, serikali imewatuliza wananchi kwa kusema imeamua kuwanyang’anya vyeti makandarasi wa aina hiyo.

Katibu wa kudumu katika Wizara ya Ajira, Musonera Gaspard, amesema serikali haitoendelea kuwafumbia macho makandarasi wasio na sifa ambao huishia kuwadhulumu vibarua.

Miongoni mwa hatua ambazo amesema zitachukuliwa dhidi yao, ni kuwanyang’anya vyeti ili wasiweze kupata zabuni zozote zile za taasisi za serikali.

“Tutakuwa tunawanyang’anya vyeti na tutawabana wasipate vibali vya kufanya kazi zingine kutokana na udhalimu wao,” Bw Musonera amenukuliwa na Kigali Today.

Ili kufanikisha jambo hilo, Bw Musonera amesema serikali itashirikiana na watendaji wa wilaya zote wanaohusika na masuala ya ajira, yaandikwe majina ya makandarasi wanyang’anyi.

Habyarimana Vénuste amesema muuza duka ameshikilia baiskeli yake aliyoweka rehani baada ya kusubiri malipo ya ujenzi wa Jengo la Wilaya ya Bugesera na kuambulia patupu.

“Tumetoka kapa na bila shaka watawadhulumu na wengine kwingineko, tutafurahi kama watachukukuliwa hatua,”ameongeza Bw Habyarimana.

Baadhi ya makandarasi wamekuwa wakiinyooshea kidole serikali kuwa inachelewa kuwalipa na hivyo kusababisha na wenyewe wachelewe kuwalipa vibarua wao.

Makandarasi wamesikika pia wakiitaja mirungura wanayolazimika kutoa ili kupata zabuni, kuwa inawafanya wapate hasara na hivyo kupelekea wasiweze kuwalipa vibarua wao ipasavyo.

Weka maoni