Serikali ya Rwanda yapuuzia mbali vilio vya manesi mitihani migumu

322
Waziri anayehusika na huduma ya afya ya msingi nchini Rwanda, Ndimubanzi Patrick.

Wizara ya Afya nchini Rwanda (MINISANTE) imesema vilio vya manesi wanaosema mitihani ya lazima wanayopewa kabla ya kuruhusiwa kufanya kazi ya unesi, haina misingi ya kueleweka.

Manesi wamekuwa wakisema mitihani hiyo ambayo wanalazimika kupasi ili kupata kibali cha kufanya kazi ya unesi nchini, ni migumu na inakuwa imesheheni maswali kuhusu vitu ambavyo hawajasomea.

Juzijuzi baraza la manesi lilitoa matokeo ya mitihani husika ambayo kati ya manesi 1231 waliotahiniwa, 171 tu ndio walifuzu huku wengine 917 wameshindwa.

Baraza la manesi limesema mitihani hiyo inazingatia mambo ambayo manesi huwa wamesomea shuleni, na wala si migumu kama manesi wanavyodai.

Waziri anayehusika na huduma ya afya ya msingi, Ndimubanzi Patrick, amelazimika kujitokeza bungeni kutoa maelezo kuhusu mitihani hiyo ambayo imezua mijadala katika vyombo vya habari.

Bw Ndimubanzi amesema mitihani hiyo haina walakini, na serikali haiwezi kuruhusu manesi uchwara wafanye kazi kwani wanaweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

“Kama anayekutibu hana uwezo na kitu anachokifanya maisha yako atayaweka hatarini, kwa hiyo tusipowatahini hatutajua kama wana uwezo au la,” amesema Bw Ndimubanzi.

Amesema kuna vyuo vingi vinavyofundisha unesi ambavyo si rahisi kujua kama vinatoa elimu ambayo imekidhi wiwango vya ubora, hivyo kuna sababu ya kuwatahini manesi hao ili kupima uwezo wao.

Aidha, baraza la manesi limesema wapo ambao katika shule za sekondari walisomea vitu ambavyo havihusiani na unesi kama ualimu na hata ujenzi, ambavyo huwafanya wasipasi mitihani hiyo.

Hiyo imetajwa kuwa ndio chanzo cha baadhi yao kushindwa kujua ulipo moyo katika mwili wa binadamu.

MINISANTE imesema hivi karibuni itashauriana na Wizara ya Elimu (MINEDUC) na Baraza la Vyo Vikuu (HEC) wahakikishe kwamba wote wanaosomea unesi walisomea sayansi katika shule za sekondari.

Weka maoni