SportPesa kumleta beki wa Arsenal nchini Tanzania

114

Vichwa vya watanzania bado vina masalia ya ziara ya Wayne Rooney na Everton Wakati bado watu wanakumbuka juu ya ziara hiyo kuna taarifa ya ujio mwingine mkubwa nchini kwa udhamini wa SportPesa.

Ikiutumia vyema ushirika wake na vilabu vya EPL, SportPesa sasa inamleta nguli na balozi wa klabu ya Arsenal kutoka jijini London ambao ni mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Uingereza huku pia wakiwa ni mabingwa wa kihistoria wa kombe la FA ambao wamelitwaa mara 13.

Ujio wa Sol Campbell nchini Agosti 5 mwaka huu ni mwanzo wa ushirika kati ya klabu ya Arsenal na Tanzania kupitia kampuni ya SportPesa ambao ni washirika rasmi wa Arsenal katika michezo ya kubashiri kwa bara la Afrika.

Arsenal na SportPesa waliingia mkataba wa miaka mitatu na nusu ambao utaishuhudia klabu hiyo ya Arsenal ikileta maofisa wake wa benchi la ufundi kwa ajili ya kuendesha kliniki za soka kwa makocha na wachezaji barani Afrika na tayari wameshafanya hivyo mara kadhaa nchini Kenya.

Atakapokuwa nchini, Sol Campbell atapata nafasi ya kutembelea klabu ya michezo ya walemavu ya Muungano na kubadilishana nao mawazo na kisha siku ya tarehe sita pia atatembelea shule ya soka ya Magnet katika viwanja vya Gymkhana ambapo atapata nafasi ya kukutana na wachezaji chipukizi, kucheza nao na pia kuwapa hamasa katika safari yao ya soka.

Kubwa zaidi ni pale ambapo Campbell ataongoza jopo la wapenzi wa klabu ya Arsenal nchini kutazama mechi ya Ngao ya Hisani siku ya Jumapili ya Agosti 6 kati ya klabu ya Arsenal ambao ni mabingwa wa FA dhidi ya Chelsea ambao ni mabingwa wa EPL.

Ikumbukwe kuwa Arsenal ni klabu inayoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi nchini Tanzania hali kadhalika barani Afrika. Hivyo naona jinsi ambavyo ujio huu wa Sol Campbell unavyotimiza ndoto za kundi kubwa la mashabiki wa soka nchini.

Sol Campbell alijiunga na Arsenal mwaka 2001 akitokea klabu ya Tottenham Hotspurs ambaye aliiongoza safu ya ulinzi ya klabu ya Arsenal kucheza mechi 49 bila kufungwa huku pia wakiweza kutwaa ubingwa wa EPL kwa msimu wa 2003-2004. Campbell aliondoka Arsenal mwaka 2006 na kujiunga na Portsmouth na nchini Uingereza pia kabla ya kurudi klabu ya Arsenal kwa mara ya pili mwaka 2009 baada ya walinzi William Gallas na Thomas Vermalen kuumia.

Weka maoni