T-Rock aachia video ya wimbo wake wa My Number One aliomuiga Diamond

487

Msanii T-Rock Saxo ameachia video ya wimbo wake wa My Number One unaomsifia Rais Paul Kagame kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 4, 2017.

Ni wimbo ambao T Rock alimuiga beat na melody nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz. Ujumbe tu ndio tofauti kati ya My number One wa T-Rock na My Number One wa ‘Simba’.

“Nimetunga huu wimbo kwa misingi ya mafanikio ya Mheshimiwa Rais Paul Kagame ambaye aliwafanyia mema Wanyarwanda ikiwemo kutamatisha mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi na kupigania ustawi wa jamii. Ni mkombozi, ni shujaa, mfano wa kuigwa na baba kwangu,” amesema T-Rock Saxo.

Msanii huyo amesema amekuwa akijaribu kuwasiliana bila mafanikio na Diamond Platnumz ili amuombe idhini ya kutumia wimbo huo kwa maslahi yake.

Amesema alifanikiwa kuipata namba ya rununu ya Diamond Platnumz ila mara zote akipiga huwa hapokelewi, lakini bado anamtafuta kwa bidii na ana imani ipo siku atampata.

“Kuna watu wengi niliwaomba waniunganishe na Diamond, namba yake niliipata ila sijafanikiwa kuongea naye, ilibidi nimuombe hadi Chege wa TMK msaada wa kumpata Diamond ila hakunisaidia chochote, kaniambia tu eti kama nataka muziki wangu upande hadhi upate kujulikana kimataifa natakiwa nifanye kazi nzuri tu zenyewe zitajitangaza, kaniambia hata yeye anajulikana Rwanda ilhali hafahamiani na mtangazaji hata mmoja wa Rwanda kwa maana kwamba kazi zenyewe hujifanyia matangazo,” amesema T-Rock katika mahojiano na Habari Pevu.

My Number One ni wimbo unaoyazungumzia maendeleo ya Rwanda chini ya uongozi wa Rais Kagame aliyeongoza majeshi ya RPA yaliyoikomboa Rwanda kutoka mikononi mwa serikali ya MRND iliyoratibu na kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja katika kipindi cha miezi mitatu tu, Aprili-Julai 1994.

Video yake imetengenezwa na timu ya wataalam wa masuala ya video wa RBA (Rwanda Broadcasting Agency) wakiongozwa na Robert Makena.

Unaweza ukaangalia wimbo wa CCM Number One wa Diamond Platnumz ambao aliutunga kwa lengo la kukinadi Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimekuwa madarakani nchini Tanzania tangu kiundwe mnamo mwaka 1977.

Weka maoni