Tanzania: Wabunge waliotajwa kutekwa waanza kuchukua tahadhari

127
Baadhi ya wabunge waliotajwa kuwa wanasakwa ili watekwe

Taarifa ya Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, kuwa wabunge 11 wamo katika orodha ya watu wanaoweza kutekwa wakati wowote imesababisha waliotajwa kurekebisha mienendo yao kuepuka kunaswa huku wakisema hawana hofu.

Bashe, ambaye alisema kuwa alitekwa na maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, aliliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa kuna wabunge ambao bado wanasakwa na maofisa hao.

Mitandao ya kijamii iliichukua taarifa hiyo na kuiongezea nyama, ikiwataja wabunge hao kuwa ni Bashe, Aeshi Hilaly (Sumbawanga Mjini-CCM), Mwita Waitara (Ukonga-CHADEMA) na Tundu Lissu (Singida Mashariki-CHADEMA).

Wengine ni Mwigulu Nchemba ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Zitto Kabwe (Kigoma Mjini-ACT) na Nnape Nauye, mbunge wa Mtama kwa tiketi ya CCM ambaye alitishiwa bastola na askari kanzuwakati akielekea kuzungumza na waandishi wa habari baada ya kuvuliwa uwaziri.

Wakizungumza na Mwananchi, wabunge hao walisema tangu kutajwa kuwa wanasakwa wameanza kuishi kwa tahadhari.

“Nimeanza utaratibu wa kutoa taarifa ya sehemu ninayokwenda,” alisema Bashe.

“Lakini vitishi hivyo haviwezi kubadilisha mfumo wangu wa maisha wala kubadilisha ninachokiamini.”

Bashe alisema alilazimika kulizungumzia suala hilo bungeni kwani kwa kuwa vitisho si dhidi yake pekee, bali wabunge wengine na Watanzania kwa ujumla.

Mbunge mwingine ambaye amesema ameanzisha utaratibu kama wa Bashe ni Aeshi, ambaye amesema anapiga simu kuwaeleza watu wake wa karibu sehemu anapoenda baada ya kutishiwa uso kwa uso na kiongozi wa serikali mkoani Dar es Salaam.

“Mwenzako tangu nitishiwe na yule kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, nimekuwa nikiishi kama popo na kila sehemu ninapoenda napiga simu kwa watu mbalimbali kuwaeleza sehemu nilipo. Hata kwenye simu yangu nimetegesha (GPS) kwa ajili ya (wengine) kujua eneo nilipo,” alisema Aeshi.

Lakini Waziri Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, alisema hakuna kitu kama utekaji na kuwataka wabunge wenzake kuondoa hofu.

“Ngona nikuambie, kwanza hakuna kitu kama hicho, pia hakuna sababu kama hiyo, na tatu nchi yetu haijafika katika hatua kama hiyo,” alisema Mwigulu.

“Nadhani ama hofu au watu wenye nia ya kutengeneza taharuki za kutaka kuchafua nchi yetu. Kwa maana hiyo mimi kama waziri ninayeshughulikia masuala ya usalama kwa raia kwa ujumla ninawaambia hakuna kitu kama hicho.

Mbunge mwingine aliye kwenye orodha hiyo, Zitto ambaye aliwahi kuamua kutotoka viwanja vya Bunge hadi usiku aliposaidiwa na Spika baada ya kupata taarifa za kukamatwa, amesema kumekuwa na taarifa kama hizo mara nyingi.

“Mwaka jana niliambiwa kuwa wabunge tunaowindwa tupo watatu, mwanzoni mwa mkutano huu wakawa saba. Wakati huu wa Bunge na Bajeti nikajulishwa kuwa tumefikia saba. Sasa naona idadi iliyotangazwa na mheshimiwa Bashe inasema ni wabunge kumi na moja wanaotakiwa kutekwa,” alisema Zitto.

“Nadhani ni mambo ya kupeana hofu tu. Kwanza, sijafanya lolote la kusababisha nitekwe, kuteswa na kupotezwa. Hivyo habari hizi nazidharau kwa sababu sioni sababu kwa nini nitekwe.”

Naye Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga, alisema ameanza kuishi kwa hofu baada ya kupata taarifa kuwa anasakwa ili atekwe.

“Maisha yangu ni ya wasiwasi kwa sababu mtoa taarifa anasema hao watu wanaotaka kutukamata wapo 14. Wameelekezwa waje Dodoma na sehemu wanayotuvizia ni kwenye geti la kutokea bungeni,” alisema Waitara.

Chanzo: Mwananchi

Weka maoni