Tatizo la watoto wanaobebeshwa mimba Rwanda bado ni pasua kichwa

200
Waziri wa Usawa wa Jinsia na Maendeleo ya Familia, Espérance Nyirasafari (kulia) na Gatsinzi Nadine ambaye ni Katibu wa Kudumu katika wizara hiyo (Picha/Igihe)

Watoto wa kike wapatao 17,500 walishika mimba zisizotarajiwa mwaka jana tu, waziri wa usawa wa jinsia na maendeleo ya familia nchini Rwanda amesema.

Waziri Espérance Nyirasafari amesema baadhi ya wasichana hao ni watoto wa shule ambao walilazimika kukatisha masomo, kwa mujibu wa Igihe.

Bi Nyirasafari alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 mbele ya kamati ya bunge inayoihusika na masuala ya bajeti na hesabu za serikali.

Bi Nyirasafari amesema idadi ya wasichana waliopewa ujauzito mwaka uliopita inatisha, na kuahidi kuwa serikali itachukua mikakati kabambe dhidi ya wanaume waliowanyanyasa.

Mbunge Mpiranyi Théobald aliitaka serikali ilitafutie ufumbuzi haraka iwezekanavyo tatizo hili la wasichana wadogo wanaolaghaiwa na wanaume wakomavu na kuwaingilia kingono.

Ameongeza, “Kuna shida nimeiona mimi, katika ripoti aliyotuonesha waziri, walioshika mimba wakiwa na miaka 16 na 19 mwaka mmoja tu waliozaa ni zaidi ya elfu 17, bila shaka hili ni tatizo nyeti ambalo inabidi tulijadili na kuangalia jinsi ya kulitatua.”

Waziri Nyirasafari amesema wizara anayoiongoza inahitaji uungaji mkono wa vyombo vya sheria na wizara ya afya, ili wanaume waliohusika na vitendo hivyo vya kuwapa mimba wasichana wadogo wapandishwe kizimbani.

Utafiti uliofanywa na muungano wa mashirika ya kutetea haki za binadamu (CLADHO) mwaka jana, ulionyesha wazi kwamba watoto 818 walio na umri wa miaka chini ya 18 walipewa uja uzito na watu wakubwa tena ambao ni wanafamilia wao.

Mbunge Munyangeyo amesema tatizo husika lazima lichukuliwe kama tatizo sugu kwani limekuwa likionekana kwa miaka mingi bila kupatiwa ufumbuzi wa kueleweka.

Waziri Nyirasafari amependekeza kushikiliwa mali za wanaume wanaowabebesha mimba watoto wa kike, ili mali hizo zitumike kuwasaidia watoto hao ambao wengine huwa ni maskini hohehahe.

Rwanda ni nchi ambayo ina wakazi wanaokadiriwa kuwa ni 445 kwenye kilomita moja ya mraba.

Weka maoni