The Adams Cool Family wayatembelea tena makumbusho ya mauaji ya kimbari

979
Mashabiki wa Dj Adams wakipiga picha ya pamoja kabla ya kuingia makumbushoni
Dj Adams

Dj Adams alizizolea umaarufu nchini Rwanda kama mtangazaji aliyesimama kidete kuwakosoa wasanii wa Rwanda, ambapo alisikika mara kibao akiwaita wasanii uchwara.

Mazoea yake ya kuwachana wasanii wenye kasumba ya kuimba kwa kufuatisha CD huku wengine wakiiga nyimbo za watu bila kuwa na idhini, yalimpa mashabiki na maadui.

Wapo wasanii kama Tom Close ambao walimpa makavu wakimuita mzinguaji ila hakuonekana kukatishwa tamaa na matusi yao ambapo aliwabishia kwa mikausho mikali isiyo na majuto.

Upekee wake katika kubingirisha gurudumu la maendeleo ya muziki ulimsababishia mazingira magumu na mazuri pia. Baadhi ya wadau wa muziki walimchukia huku wengine wakimpongeza.

Alitangazia redio nyingi ikiwemo City Radio na Redio One. ‘The Drive Show’ na ‘The Red Hot Furahi Day Night’ ni miongoni mwa vipindi vyake vilivyokuwa na usikivu mkubwa.

Mwaka 2014 wapenzi wa vipindi vyake walifikia hatua ya kuunda kundi la The Adams Cool Family, ambalo hata baada ya yeye kurudi Kenya alikozaliwa Januari 7, 2017, liliendelea kuwepo.

Kuyatembelea makumbusho ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja, ni miongoni mwa vitu wanavyovipa kipaumbele katika maisha yao.

Wikiendi iliyopita waliyatembelea Makumbusho ya Kigali yaliyoko maeneo ya Gisozi. Miaka miwili iliyopita waliyatembelea Makumbusho ya Ntarama na yale ya Nyamata wilayani Bugesera.

Wanakundi wa Adams Cool Family wakiweka mashada ya maua kwenye kaburi huko Gisozi kunako Makumbusho ya Kigali ya Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi

“The Adams Cool Family ni kundi la watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wavulana na wasichana ambao hawakutanishwi na dini, ushabiki wa timu fulani au chama chochote kile cha siasa isipokuwa urafiki tu na ndiyo maana ikatoka kwenye kuwa wapenzi wa vipindi vyangu kwenye redio tukawa marafiki na mwishowe tukawa familia,” amesema Dj Adams katika mahojiano na Habari Pevu.

“Kwa kweli mimi DJ Adams siyo manusura wa mauaji ya kimbari na wala sina ninayemjua kwenye familia yangu ya kidamu aliye manusura. Lakini mimi ni Mrwanda na kila aliyeathirika na mauaji ya kimbari ni ndugu yangu kwa namna moja ama nyingine, na nchi kwa ujumla iliathirika na ni nchi yangu,” ameongeza Dj Adams ambaye jina lake halisi ni Adam Aboubakar Mukara.

Pamoja na kwamba Dj Adams hayupo Rwanda, mashabiki wake hawakuvunja umoja wao bali waliongeza urafiki kwa ajili ya maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla, kama wanavyosema.

“Desturi za kundi ni kuangalia ni kipi kinaweza kusaidia vijana wenzetu na nchi pia,”amesema Ramadhani Sindayigaya ambaye ndiye mratibu wa Adams Cool Family.

“Umuhimu wa kuyatembelea maeneo yanayohifadhi historia ya mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi ni kufika na kuangalia kilichotokea huku Rwanda, kuna wazee waliuawa, mtoto ambaye hajafanya baya lolote lile, mtoto huyo akiuawa nchi imepoteza kitu kikubwa. Haiingii akilini unaua hadi mtoto wa mwezi mmoja na hata wale ambao walikuwa bado wapo kwenye tumbo za mama zao,” ameongeza Bw Ramadhan kwa msisitizo.

Aidha, wanakundi wa The Adams Cool Family wapatao 35 husaidiana wakati wa dhiki kwa mfano mmoja wao akifiwa au kuugua, kwa mujibu wa maelezo ya Bw Ramadhan.

Alipoulizwa wanavyoweza kudumisha umoja wao wakati yupo Kenya Dj Adams ametoa jibu hili: “Si lazima niwe niko Rwanda ili tupange kuwatembelea wagonjwa, wajane, tuende kwenye makumbusho ya mauaji ya kimbari na kadhalika. Kwa uaminifu baina yetu na kila kitu ni mtandaoni mpaka tunapoamua kukutana ana kwa ana kwa ajili ya kufanya kitu fulani. Alhamdulillah hakuna kitu kimewahi kuharibika kwa kuwa mmoja wetu yuko mbali. Ikiwa ni kitu kinachohitaji uwezo wa kihela tunatumia mbinu zilizopo za kutuma hela na kinachotakikana kinapatikana.”

Akiongea na Habari Pevu, Dj Adams amesema kwa sasa anaisaka kazi ya utangazaji nchini Kenya na anaamini ataipata kwani ana akiba ya lugha nyingi kuliko wakenya walio wengi.

“Wengi wanaongea lugha zisizozidi tatu wakati mimi naongea lugha zote zinazotumiwa na mataifa ya Afrika Maskariki kama Kiswahili, Luganda, Kinyarwanda, Kirundi, Kikuyu, ukiongezea Kiingereza na Kifaransa nadhani watangazaji hapa watapotea kwa lugha tu.”

Weka maoni