Tisa mbaroni kwa kuvunja nyumba, wizi

295

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza nchini Tanzania linawashikilia watu tisa kwa tuhuma za kujihusisha na uvunjaji wa nyumba na kuiba mali wilayani Ilemela.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema watu hao walikamatwa kutokana na doria na msako wa watu wanaojihusisha na uvunjaji wa nyumba usiku na kuiba mali iliyoanza Aprili 9, mwaka huu.

Alisema askari walifanya operesheni hiyo katika Kata ya Kirumba likiwamo soko la Kirumba, Kitangiri, Nyamanoro, Pasiansi, Ibungilo na Kawekamo wilayani Ilemela baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Alisema katika operesheni hiyo pia ilikamatwa mali na vitu mbalimbali zikiwamo runinga, kwa mujibu wa Gazeti la Mtanzania.

Msangi alisema watuhumiwa wote wanahojiwa na jeshi la polisi na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani huku msako waa kuwakamata wahalifu wengine wa aina hiyo unaendelea.

Kamanda aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mwanza kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu mapema waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Weka maoni