Umaskini na lugha ndivyo vinafanya tusijulikane kimataifa – Oda Paccy

929
Oda Paccy, moja kati ya marapa mahiri wa kike nchini Rwanda (Picha/Inyarwanda)

Hata kujulikana nchini inakuwa si rahisi kwa wasanii wanaochupukia, ila ukitaka kutoboa mipaka kupata umaarufu wa kimataifa unasota zaidi, amesema rapa Odda Paccy.

“Mnyarwanda nikiimba kwa Kinyarwanda ananielewa kirahisi na anaupenda muziki wangu japo msanii chipukizi anatakiwa ajitume sana ili wapate kutambua kipaji chake, ila kuja kujulikana nje ya Rwanda ndipo linakutoka jasho jingi,” amesema rapa huyo wa kike Odda Paccy katika mahojiano na Habari Pevu.

“Ugumu upo hasa upande wa uwezo wa kipesa, sababu za kutojulikana nje ni nyingi ila suala la uwezo wa kifedha ndo linatutesa zaidi,” ameongeza hitmaker wa Ese nzapfa na Miss President.

Ametoa mfano wa wimbo wake mpya wa Nobody aliotengenezewa Wasafi Records, Tanzania, mapema mwaka huu, ambapo gharama ya audio na video imefikia faranga miliyoni 4 ambayo “ni hela kubwa ipatikanayo baada ya msanii kutaabika” hasa kwa wale ambao hawana wadhamini kama yeye.

Oda Paccy amesema udogo wa eneo wa Rwanda ambao ni kilomita 26,338 za mraba na uchache wa raia ambapo raia wa Rwanda ni miliyoni 12 tu, navyo huwafanya wasanii wa Rwanda wasipate maendeleo kama wasanii wa mataifa makubwa kieneo na ambayo yana raia wengi kwani raia ndio wateja wa kazi za wasanii.

Aidha msanii huyu wa kike amesema ingawaje hizo ndizo changamoto kubwa, ila “lipo hata suala jingine gumu la lugha ambayo wasanii wa Rwanda tunatumia, Kinyarwanda ni lugha ya Wanyarwanda tu.”

Amesema huwezi kutegemea kupata maendeleo makubwa wakati unaimba kwa lugha ambayo inazungumzwa na watu wachache. “Mtanzania akiimba Kiswahili tunaelewa anachoimba kwani Kiswahili si lugha ya watanzania tu hata sisi tunakijua, ila mimi nikiimba Watanzania hawaelewi chochote,” ameongeza Paccy.

Amesema hiyo ndiyo ilimfanya aridhie ushauri wa kuyabadilisha mashairi ya wimbo wake wa Nobody alipofika Tanzania, ambapo awali alikuwa ameyatunga kwa Kinyarwanda.

“Waliniambia naimba vizuri ila wakanishauri nitafsiri mashairi kwenda Kiswahili na Kiingereza nikafanya hivyo kwani hata mimi najua Kinyarwanda ni lugha yangu na naipenda sana ila sitaki iharibu ndoto zangu za muziki za kuwa msanii wa kimataifa,” ameeleza Paccy.

Oda Paccy amechukua nafasi hiyo kuwashukuru Watanzania waliompa shavu kwa namna moja ama nyingine mapema mwaka huu alipoenda Tanzania katika juhudi za kutanua muziki wake ambapo amesema walimshughulikia kwa ukarimu kana kwamba walikuwa wanajuana naye ilhali ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kufika Tanzania na wala hakuwa amepiga siku mapema kuomba kupokelewa Wasafi Records.

Amemshukuru hasa Leizer aliyemtayarishia wimbo wake huo wa Nobody, na Khalifan ambaye alisimamia uongozaji wa video, na kusema wimbo huo umempandisha cheo kingine kwenye ulingo wa muziki wa Afrika Mashariki kwani ukiacha jinsi unavyopigwa nchini Rwanda hasa maredioni na kwenye vilabu vya starehe, hata televisheni za kimataifa kama MTV zimeanza kuucheza.

“Lengo langu ni kusambaza ujumbe si kwa Wanyarwanda tu bali kwa Afrika nzima, kwa hiyo natakiwa nijiongeze, ndiyo maana nikaenda Dar es Salaam, natakiwa nifanye muziki mzuri ambao umekidhi vigezo vya ubora na Wasafi ni studio ambayo ina hadhi kubwa kwa Afrika Mashariki, muziki mzuri najua unahitaji mtonyo ila nitajitahidi kuweka mambo sawa, lakini pia nitakuwa natumia hata lugha za kimataifa ili nijitangaze zaidi, si kuimba Kinyarwanda tu ambacho sisi tu ndio tunakijua,” ameongeza Oda Paccy.

Wadau wa muziki nchini Rwanda wamekuwa wakijiuliza kinachowafanya wasanii wa Rwanda wasiinuke, huku ukosefu wa ubunifu ukitajwa kuwa miongoni mwa sababu za wao kutotambulika kimataifa.

Hata wasanii ambao wameshindia tuzo kubwa nchini kwenye vinyang’anyiro vya muziki kama PGGSS (Primus Guma Guma Superstar) ambacho huandaliwa na kampuni ya East African Promoters kwa udhamini wa kiwanda cha utengenezaji vinywaji cha BRALIRWA, ambao ni pamoja na Tom Close (2011), King James (2012), Riderman (2013), Jay Polly (2014), Knowless (2015) na Urban Boys (2016) wameishia kuwa mastaa wa nyumbani tu.

Wasanii wamekuwa wakisema nchi inapokuwa ni maskini hata raia wanakuwa ni maskini na hivyo kufanya iwe ngumu kupata kipato kikubwa kutokana na muziki, huku hali hiyo ikiwafanya hata watayarishaji wa muziki wasiweze kununua vifaa muhimu wanavyovitaka kwa kuwa muziki haulipi vizuri.

Kwaya ya kisabato ya Ambasadors of Christ ndiyo wasanii wanaoongoza kwa Rwanda kwa kuwa na umaarufu wa kimataifa ambapo nyimbo zao zinajulikana nchini Kenya, Tanzania na nchi zingine. Hata ukiingia Youtube nyimbo za Ambassadors ndizo zina zimetazamwa na watu wengi zaidi.

2 Maoni

  1. dah hii ni kiboko. na waandishi wa hii website ni wanyarwanda au wabongo? nitakuwa naicheki nikiwa na muda. Mohammed Mwaipaja wa Tabora

  2. sijajua mumiliki wa wabsite hii lakini i want to congratulate him, nilizaliwa Tanzania miaka ya nyuma ila nimeanza kusahau Kiswahili, I hope hii website itakuwa inatusaidia. Na kuhusu Oda asikate tamaa ipo siku nyota yake itawaka, anatakiwa afanye muziki kama biashara awe mwekezaji siyo analala hajapanda halafu anasubiri kuvuna. utavuna ulichopanda.

Weka maoni