Upungufu wa magari ya abiria Kigali bado ni pasua kichwa

560
Foleni ndefu za abiria wakisubiri magari Kigali mjini kati

Upungufu wa magari ya abiria jijini Kigali unatajwa kuwa kikwazo kikuu kwa wakazi wa jiji hilo.

Mara nyingi utawakuta raia wamepanga milolongo mirefu ya mistari, wakisubilia magari ya kuwapeleka sehemu moja hadi nyingine.

Hatua hiyo imekuwa ikiwachelewesha watu kufika sehemu wanapokuwa wamekusudia kuwepo.

Kituo cha mabasi yaendayo majimboni na nje ya nchi cha Nyabugogo

Milolongo mirefu ya watu wanaosubiri magari katika vituo kadhaa vya mabasi jijini hapa, siku hizi siyo jambo geni.

Kuna wanaodai kuwa tatizo hili limeongezeka siku hizi za karibuni.

Muda mwingine abiria husubiri hadi masaa kwa safari za ndani ya mji wa Kigali.

“Magari hayatoshi, kila wakati iwe asubuhi, mchana na hata jioni watu lazima wawe wako kwenye mistari, magari yaliyopo hayaotoshi ukilinganisha na abiria waliopo,” amesema dereva mmoja tuliyemkuta Nyabugogo.

Miaka ya nyuma ukosefu wa magari ya abiria haukuwa kama ilivyo sasa.

Baadhi wanadai tatizo limeanza kushamiri pale uongozi wa jiji la kigali ulipoamuru kila basi liwe na mashine zinazokata pesa kutoka kwenye kadi ya abiria, huku wengine wakidai limezidi kuwa kero kufuatia ujenzi wa barabara jijini kigali ambao hulazimisha magari kupita barabara zingine ambazo hazikuzoeleka.

Mmoja wa madareva ambao tumeongea naye maeneo ya Nyabugogo

Lakini je, ukweli wa jambo hili ni upi? Na ni nini kinachofanywa ili kudhibiti hali hiyo ?

Busabizwa Parfait ni kaimu meya wa jiji la Kigali. Amesema “Mashine zile siyo chanzo, bali makampuni ya kusafirisha abiria jijini hapa yana upungufu wa magari, lakini mabasi mengine yameshanunuliwa, kwa hiyo wiki ijayo magari yasiyopungua 60 yatamwagika jijini hapa. ”

Mwezi uliopita rais Paul Kagame alipewa tuzo ya mjenzi mkuu baada ya kutajwa kwamba, amewezesha mji wa kigali kuwa mji usafi kuliko miji yote barani Afrika.

Lakini pamoja na hayo usafi huu unatakiwa uendane na mahitaji mengine kama vile uwingi wa mabasi ya abiria ili kuwawezesha wakazi wa jiji hili kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa urahisi.

Weka maoni