Urban Boys hatarini kusambaratika

244
Kutoka kushoto: Nizzo, Humbe na Safi

Kundi la muziki wa RnB na Afropop nchini Rwanda la Urban Boys liko hatarini kugawanyika kutokana na memba wake mmoja Safi kujitoa kwenye kundi hilo.

Baada ya Safi kutangaza kujitoa kutokana na kundi “kuonekana kutokuwa na mwelekeo”, wadau wa muziki wanajiuliza kama kundi litaendelea kuwepo kwani ndiye alikuwa muimbaji muhimu.

Dalili za kundi hili kuingia pabaya zilianza kudhihirika baada ya Safi kutomualika Nizzo kwenye harusi yake iliyofanyika mapema mwezi jana, ambapo Nizzo alisema hakualikwa na asingekwenda harusini kama mzamiaji, huku akisema kuna miaka miwili hapigiani simu wala jumbe na Safi.

Baadaye Safi alisema hakuona sababu ya kumualika Nizzo kwani alimchukulia kama ndugu yake tena wa karibu ambaye hakutakiwa kusubiri kualikwa wakati harusi ni ya mwenzake.

Safi amemuambia mtangazaji Epa Ndungutse wa Redio Rwanda kwamba yeye na wenzake (Humble na Nizzo) walikuwa wameshindwa kuelewana kuhusu miradi ya kundi mpaka kupelekea meneja wao Richard kuwapa kisogo.

Safi amesema amesikitika kuwaaga wenzake ili kufanya muziki wa solo, akisema amechukua uamuzi huo shindo upande, baada ya kuona kundi halina mipango na hata maelewano ya wanakundi kufifia.

Amesema msuguano huo ndio ulisababisha watoe nyimbo mbili tu mwaka huu ambazo ni Mama na Nipe, kinyume na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wanaachia albamu kila mwaka.

Angalia video ya Nipe, wimbo waliomshirikisha Ykee Benda kutoka Uganda.

Urban Boys ni kundi ambalo lipo kuanzia mwaka 2007 ambapo lilianzishwa huko Butare Kusini mwa Rwanda kabla ya kuhamia Kigali miaka miwili iliyofuatia.

Baada ya Safi kutangaza kujivua uanakundi, mustakbali wa kundi umeingia mashakani, licha ya Nizzo kudai kuwa hata na Humble ajitoe yeye ataendelea kuwa kundini akisema hawezi kulitelekeza kundi ambalo aliliasisi yeye.

Safi na Humble wakiwa kwenye ndege wakienda tamashani ughaibuni

Huku kiza kinene kuhusu mwelekeo wa kundi kikiendelea kutanda, Safi amejimilikisha akaunti ya Youtube ambayo ilizoeleka kuwa ni ya kundi zima.

Akaunti ambayo ilikuwa inaitwa Urban Boys Official iliyoundwa mwaka huu ambayo kwa sasa imesheheni ngoma nne ikiwemo wimbo mmoja ambao Humble alishirikiana na mpenzi wake tu, Safi ameibadilishia jina na kuiita Safi Madiba Official.

Kitendo hicho kimewakasirisha Humble na Nizzo ambao wameonekana kuumia sana ukiangalia maneno yaliyojawa na hasira ambayo wameandika Instagram wakimtaka aondoke yeye kwa amani bila kupora miliki za kundi.

Humble ameposti screenshot ya muonekano wa akaunti mpya hiyo na kuisindikizisha mpasho: “No no uporaji haufai tafadhali.”

No no gusahura ntabwo aribyo plz @safimadiba_official

A post shared by humble jizzo (@humble_jizzo_urbanboys) on

Inatarajiwa kuwa Novemba 10 kutakuwa na kikao na waandishi wa habari ambacho kimeitishwa na Humble kikiwa na lengo la kuweka bayana hatma ya kundi hilo ambalo limejizolea umaarufu wa kitaifa.

‘Mama’ ndio wimbo wa mwisho ambao Urban Boys walitoa wakiwa watatu. Ikumbukwe kwamba wimbo wao wa kwanza walioutoa wakiwa watatu unaitwa Icyicaro kwani kundi lilianza likiwa na memba watano.

Angalia video ya Mama

Weka maoni