Video: Mfungaji bora wa Uganda Frank Karanda ahamia AS Kigali

276

Mfungaji bora wa ligi ya Uganda, Frank Karanda ametua mjini Kigali mchana wa leo Jumatatu, kwa ajili ya mkataba wa miaka mitatu anaotarajiwa kuingia na klabu ya As Kigali.

Timu ya AS Kigali ambayo ipo nafasi ya nne katika ligi kuu ya Rwanda ndiyo iliyomtumia tiketi ya usafiri wa ndege, kwa mujibu wa wakala wake Patrick Gakumba.

Kuhusu malipo na masharti ya kazi, Karanda amewaambia waandishi wa habari kwamba pande mbili zimeshafikia mwafaka na anakuja kumwagia wino mkataba ambao umeshaandaliwa tayari kuanza kuichezea timu hiyo.

Frank Karanda alijizolea sifa nyingi nchini Uganda hasa baada ya kujinyakulia tuzo ya mfungaji bora kwa misimu miwili mfululizo katika ligi kuu nchini humo.

Msimu uliopita alitwaa tuzo ya mfungaji bora baada ya kujihakikishia magoli 18 huku msimu uliotangulia alifua dafu kuzitikisa nyavu mara 23.

“Ujio wa mfungaji stadi wa Uganda unaashiria kuimarika kwa ligi ya Rwanda, halafu mnajua timu ya Uganda inavyofanya vizuri, majuzi mliona ilivyoichabanga Cape Verde,” amesema Patrick ambaye ni wakala wa Karanda.

Ameongeza “Kadri Rwanda inavyozidi kupata maendeleo ni lazima hata kwenye michezo tuende mbele, kwa hiyo mimi ningependa kusisitiza kwamba timu itakayochukua ligi mwaka 2018 itakuwa ni timu ambayo imevifanyia kwa sababu mpaka sasa hivi wachezaji wote wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu wanazidi kuja Rwanda, hiyo inaonesha sura nzuri ya Rwanda na sura nzuri ya michezo.”

Patrick ambaye ni wakala wa kimataifa wa wachezaji na makocha, amejizuia kuzungumzia dau la uhamisho wa mteja wake na hata mshahara atakaokuwa analipwa, akisema hiyo ni siri ya kazi.

“Dau lenyewe siku zote mimi nasema ni siri ya mchezaji, nisije nikatangaza wakampiga mapanga uwanjani bhana,” amesema Patrick kwa msisitizo.

Karanda amekataa katakata kuzungumzia maudhui ya mkataba anaokuja kusaini na kuwataka waandishi wa habari wamuulize wakala wake ambaye na yeye hakutaka kuangazia suala hilo.

“Mimi ningependa niseme kwamba atalipwa mshahara mnono na amefurahi ndiyo maana ameacha timu yake ya Uganda amekuja hapa, kwa hiyo anachokuja kufanya ni kufanya hamasa Afrika Mashariki ijue kwamba Wanyarwanda wanasajili wachezaji kutoka sehemu zote kwa sababu kama Congo iko huku, Burundi imekuja, umeona Waganda wamekuja na wengine watakuja,” ameeleza Patrick.

Weka maoni