Video: STES-Rwanda wazindua gari la kutumia umeme jua

1268

Wanafunzi 12 wa Chuo Kikuu cha Singhad Technical Education Society – Rwanda (STES-Rwanda) wametengeneza gari linalotumia nishati ya mionzi ya jua.

Waandishi wa habari leo hii wameonyeshwa gari hilo ambalo linafanyiwa umaliziaji, na kupewa maelezo kuhusu uwezo wake kabla dereva hajaingia ndani yake kuliendesha likiwa limembeba yeyé na abiria wawili.

Ni gari litakalosaidia kupambana na tatizo na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na moshi wa magari yatumiayo mafuta, kwa mujibu wa muasisi wa STES-Rwanda, Nzitonda Kiyengo.

“Gari hili halitoi moshi kwani lenyewe linatumia umeme wa mionzi ya jua, halafu pia watu wana kila sababu ya kulitumia kwani halihitaji mafuta na mnajua mafuta yalivyo ghali,” ameongeza.

Wanafunzi 10 wa chuo hiki cha elimu ya Engeneering waliibuka kidedea kwenye mashindano ya utengenezaji magari yatumiayo mionzi ya jua mwezi jana huko India.

Walipofika Rwanda wakatengeneza gari kama hilo ambalo wameonyeshwa waandishi wa habari leo, na litafanyiwa maonyesho katika sherehe za kuadhimisha sikukuu ya ajira Mei 1.

“Gari hili lina uwezo wa kuenda kwa kasi ya kilomita 50 kwa saa na kutembea kwa masaa manne kabla ya kumaliza nguvu za miale ya jua kwenye betri zake,” amebainisha Bw Kiyengo.

“Vifaa vyote vilivyotumika kutengeneza gari hili tumenunua mjini hapa (Kigali) ukiacha tu usukani na magurudumu,” ameongeza muasisi wa chuo kikuu husika.

“Tunasubiri tu tupate cheti cha RSB (Shirika la Viwango Rwanda) tukishapata ndipo gari litaingia barabarani kama magari mengine na tuna uhakika hicho chetu tutapata.”

Samantha Ruzibiza, msichana ambaye ni mmoja kati ya watengenezaji wa gari hili, amesema wamefurahishwa na kazi waliyoifanya na wapo tayari kutengeneza magari mengine ya aina hii.

Akizungumzia kilichowapa motisha ya kutengeneza magari, Bw Kiyengo amesema serikali imekuwa ikihamasisha watu kuchangamkia teknolojia na hiyo ndiyo sababu kubwa.

Mbali na gari hili la kutumia nishati ya mionzi ya jua, wanafunzi wa chuo kikuu hiki wametengeneza pia mabango ya kuwaka taa usiku ambayo yanatumika mjini Kigali na Huye.

Weka maoni