Viongozi saba chini ya ulinzi kwa kujilimbikizia ng’ombe wa walala hoi Gatsibo

210
Baadhi ya ng'ombe waliotolewa kwa wasiojiweza kupitia programu ya Girinka Munyarwanda: Miliki ng'ombe Mnyarwanda)

Taarifa kutoka wilayani Gatsibo Mashariki mwa Rwanda zinathibitisha kutiwa mbaroni viongozi saba wanaodaiwa kujimilikisha ng’ombe waliotolewa na serikali kwa wananchi wasiojiweza.

Ng’ombe hao walitolewa katika programu ya Girinka (Girinka: miliki ng’ombe) inayolenga kuwatoa watu kwenye lindi la umaskini katika dhana nzima ya kuboresha lishe.

Washukiwa hao wa ubadhirifu wa mali ya umma wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Rugarama wilayani Gatsibo wakati upelelezi wa makosa yanayowakabili ukiendelea.

“Tumefanya na mkutano na raia, wametuambia walivyonyang’anywa ng’ombea wao, washukiwa wamekamatwa hapo jana Jumatano,” amesema Gasana Richard, Meya wa Wilaya ya Gatsibo.

Waliotiwa nguvuni ni Katibu Mtendaji wa Kata ya Bushobora, viongozi wawili wa vijiji huku wengine wakiwa ni watendaji wa kamati za matabaka ya kiuchumi yajulikanayo kama Ubudehe.

Wakazi wa kijiji cha Agasenga, Kata ya Bushobora, Tarafa ya Remera wilayani Gatsibo, wanadai viongozi wao walijilimbikizia ng’ombe 15 katika kipindi cha miaka mitatu tu.

Raia maskini hutengewa na serikali fungu la kima cha chini kuwawazesha waondokane na umaskini kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo za kuwapatia msaada wa mifugo.

Rais Kagame mwaka jana aliwakemea viongozi wanaobadhiri au kufuja mali ya umma, na kuwataka wawe wazalendo wasitumie vyeo vyao kuwachapia wanyonge.

Alisema mianya ya upotevu wa mali ya umma haitakiwi kuwepo, na kuwataka viongozi watambue kuwa maendeleo endelevu hayawezekani bila uchumi shirikishi.

Weka maoni