Vyama vya kiraia vitusaidie ili EAC isije ikasambaratika tena – Waziri Kanimba

256
Waziri Kanimba akiongea na waandishi wa habari leo hii mjini Kigali (Picha/Igihe)

Waziri wa Biashara na Viwanda na Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nchini Rwanda, François Kanimba amevitaka vyama vya kiraia vihusike katika mipango ya maendeleo ya EAC.

Amesema hayo leo akianzisha rasmi kikao cha majadiliano baina ya wawakilishi wa serikali na wale wa vyama vya kiraia, leo mjini Kigali, ambapo amekumbushia jumuiya hiyo ilivyosambaratika mwaka 1977.

“EAC ilisambaratika kwa sababu raia hawakuhusika katika kuratibu na kutekeleza mipango ya jumuiya, leo vyama hivi vinatakiwa vishirikiane na serikali sauti za wananchi zisikike,” amesema.

Baadhi ya waliohudhuria kikao hicho

Waziri Kanimba ametaarifu kuwa kosa ambalo lilipelekea kusambaratika kwa jumuiya ambayo miaka hiyo ilikuwa inaunganisha Uganda, Tanzania na Kenya haliwezi kujirudia.

“Leo tunatambua umuhimu wa vyama vya kiraia, hawa ndio miradi hao hutekelezwa vijijini wanajua wanachotaka raia, tunahitaji kuwasikiliza ili jumuiya isisambaratike tena,” ameongeza.

Baada ya Uganda, Kenya na Tanzania kupata uhuru, nchi hizo ziliunda Mamlaka ya Huduma za Pamoja za Afrika ya Mashariki ambapo ushirikiano huo ulihusu fedha, forodha, huduma za reli, mabandari, posta na simu na elimu ya juu.

Inadaiwa umoja huo ulilenga pia mahakama kuu ya pamoja na sera ya kiuchumi ya soko la pamoja. Haya yote yalitakiwa kuwa chini ya Bunge la Afrika ya Mashariki lakini tangu 1965 umoja huo ulianza kurudi nyuma kila nchi ilipoanzisha pesa yake.

Kutokana na tofauti zilizojitokeza kati ya mataifa hayo ambapo Tanzania iliuthamini ujamaa huku Kenya ikiupa kipaumbele ubepari wakati Uganda ikidai baadhi ya maeneo ya nchi hizo, wanachama hao walikosa ushirikiano na hivyo kupelekea jumuiya kuvunjika mwaka 1977.

Jumuiya ilikuja kufufuka mwaka 2000 kwa juhudi za marais Moi wa Kenya, Mwinyi wa Tanzania, na Museveni wa Uganda. Rwanda na Burundi zilipata uanachama mwaka 2007, miaka 9 kabla ya Sudan Kusini.

Théodore Mutabazi ni afisa anayehusika na masuala ya ushirikiano baina ya serikali na vyama vya kiraia katika Bodi ya Uongozi Bora nchini Rwanda. Amesema vyama vya kiraia vimekuwa vikitoa mchango mkubwa katika kutetea maslahi ya umma na pia kuyatafutia ufumbuzi migogoro ikiwemo mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.

Alipoulizwa kuhusu mchango wa vyama vya kiraia katika kurejesha amani na utulivu nchini Burundi, Bw Mutabazi ametoa majibu haya: “Serikali hushirikiana na vyama vya kiraia, kuna vikao vinafanyika ili kupata suluhisho hasa yakizingatiwa maudhui ya Mkataba wa Afrika Mashariki.”

Ameongeza: “Muda wote huwa tunataka vyama vya kiraia katika nchi wanachama view na ushirikiano mwema kama ushirikiano uliopo baina ya vyama kama hivyo nchini Rwanda na serikali”

Ikumbukwe kwamba Burundi imevipiga marufuku bidhaa kutoka nchini Rwanda ambapo haviruhusiwi kuvuka mipaka ya nchi hiyo kuingia Burundi, ikiwa ni baada ya nchi hizo kuingia kwenye mpasuko wa kidiplomasia unaoshuhudiwa tangu mwaka 2015.

Weka maoni