Walituzika na kuondoka wakijua hatutafufuka – Kagame

739
Ajuza akimuambia Kagame anavyompenda hapo jana Jumapili, wilayani Kamonyi (Picha zote na Urugwiro Village)

Kwa mara nyingine tena Rais Kagame ameyakemea mataifa ambayo hayakufanya chochote kusimamisha mauaji ya kimbari yaliyofanyika mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Alitoa matamshi hayo hapo jana Jumapili, wakati akipiga kampeni wilayani Kamonyi, ikiwa ni siku yake ya tatu ya kuhamasisha wananchi wampe kura zao kuelekea uchaguzi unaokaribia.

Picha hizo ambazo zimeunganishwa zinaonesha hali ilivyokuwa kwenye kampeni za rais Kagame wilayani Kamonyi

“Walitufukia shimoni na kuondoka, walitupungia mikono kutuaga, Wanyarwanda walichipuka tena kama mimea, na leo wamekomaa,” amesema Kagame, mgombea wa RPF-Inkotanyi.

Majeshi ya Umoja wa Mataifa yaliyokuwa nchini Rwanda katika operesheni ya kusaka amani mwaka 1994, yaliwatelekeza Watutsi mara baada ya mauaji ya kimbari kuanza.

Rais Kagame amewataka Wanyarwanda waungane kupambana na umaskini

Serikali ya Rwanda inalituhumu pia taifa la Ufaransa kwa kudhamini watekelezaji wa mauaji hayo yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya miliyoni moja tangu Aprili-Julai 1994.

Kagame ambaye ndiye aliyeongoza majeshi yaliyosimamisha mauaji husika, wakati wa kampeni zake amewakumbusha Wanyarwanda alichokifanya enzi hizo na kuwataka wakithamini.

Rais Kagame akiwa na mkewe Jeannette Kagame na watoto wao wawili, mmoja wa kiume Ian Kagame na binti yao Ange Kagame, wilayani Kamonyi siku ya jana.

Kiongozi huyo ambaye yuko madarakani tangu mwaka 2000, anaendelea na msako wake wa kura za wananchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 3-4 Agosti, 2017.

Kagame akisalimiana na wakazi wa wilaya ya Kamonyi kabla ya kuwahutubia

Mwaka 2015 katiba ya Rwanda ilirekebishwa kumruhusu kuwania muhula wa tatu, ambapo aliruhusiwa pia kuendelea kuongoza mpaka mwaka 2034 kama raia wataendelea kumchagua.

Wagombea wenza ni pamoja na Frank Habineza wa Chama cha Democratic Green Party of Rwanda, na Philippe Mpayimana ambaye ni mgombea huria.

Rais Kagame amesema mwenyewe kuwa atakayeshinda uchaguzi anajulikana tayari, hasa ikizingatiwa ana uungaji mkono wa vyama nane ambavyo vinampigia upatu.

PL na PSD ambavyo ndivyo vyama vinavyokipumulia kisogoni chama tawala kwa kuwa na wanachama wengi, havina wagombea bali vimeamua kumuunga mkono rais Kagame.

Katika hatua nyingine rais Kagame amekitweza chama cha Green Party kwa kusema kuwa RPF-Inkotanyi ni Green kuliko Green Party yenyewe.

Akizinadi sera zake wilayani Nyanza siku ya kwanza ya kampeni, alisema chama chake kina sera nzuri za kustawisha mazingira ukilinganisha na zile za Green Party.

Ameongeza kuwa anaamini katika siku za mbeleni wanachama wa Green Party wataihama wajiunge na chama tawala.

Rais Kagame amewataka wananchi zote wampe kura zao ili aendelee kuwaletea maendeleo kama ambayo amekuwa akiwaletea kwa miaka 17 ambayo amekuwa mamlakani.

Mabibi na mabwana walikuwa wamejitokeza kwa wingi wakiwa wameshika mabango ya kuhamasisha kumchagua Rais Kagame

Mchakato wa kampeni umeanzia Jimbo la Kusini ambapo wilaya ya Muhanga ndiyo wilaya pekee ya jimbo hilo ambayo hajafika.

Siku ya nne ya kampeni ambayo ni kesho (Jumanne), Rais Kagame atapiga kampeni katika wilaya hiyo na wilaya ya Ngororero pia ambayo inapatikana katika Jimbo la Magharibi.

Kampeni za urais zilianza mnamo Julai 14 na zitaendelea hadi siku moja kabla ya uchaguzi kufanyika.

Weka maoni