Wanasayansi wa viazi vitamu duniani wakutana Kigali

651

Wanasayansi zaidi ya 50 kutoka mabara mbalimbali wamekutana Jijini Kigali na kuanza mkutano wa siku tatu unaolenga kukuza ufahamu na uzalishaji wa viazi vitamu.

Mkutano huo wa 16 unaofanyika kila mwaka, umekuwa muda mwafaka kwa wataalam na watendaji wa  viazi vitamu kuelezea umuhimu wake katika kuboresha lishe majumbani.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kilimo Rwanda, Dkt Marc Cyubahiro Bagabe, amesema Rwanda ina kila sababu ya kushiriki juhudi za kuendeleza zao la viazi kwa kuwa vinahimili ukame.

Mwaka jana Rwanda ilikabiliwa na ukame uliosababisha mifugo hususan ng’ombe kufa kwa kukosa maji na malisho, huku mimea mashambani ikinyauka na kupelekea kuwepo uhaba wa vyakula nchini.

“Viazi vitamu huhimili ukame ukilinganisha na mazao mengine, halafu viazi vitamu hukua haraka, miezi mitatu tu huwa unaweza kuvuna, hili ni suluhisho kwa wakulima…,” amesema Dkt Cyubahiro.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kilimo Rwanda (RAB), Dkt Marc Cyubahiro Bagabe akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufungua rasmi mkutano wa wanasayansi wa viazi vitamu

Katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, utafiti katika sekta ya kilimo umetengewa faranga miliyoni moja na miliyoni mia moja, huku miundombinu kama maabara na mitambo mbalimbali inayohitajika katika sekta hiyo ikitengewa biliyoni mbili.

Mwaka ujao serikali itaendelea kuimarisha maabara ya kilimo ili kurahisisha utafiti, ambapo faranga miliyoni 200 zitatengwa kwa ajili ukuzaji wa utafiti wa viazi vitamu, kwa mujibu wa Dkt Cyubahiro.

Wadau hao wa viazi vitamu wanatarajiwa kuyatembelea maabara ya kilimo ya taifa ya ISAR-Rubona Wilayani Huye. Serikali imejipanga kutenga heka 900 kwa ajili ya kilimo cha viazi vitamu mwaka ujao.

Licha ya kuhimili ukame, viazi vitamu vinasifika pia kwa kutoshambuliwa kirahisi na magonjwa. Mwezi uliopita Rwanda ilishuhudia mahindi kuvamiwa na viua vijeshi katika wilaya mbalimbali.

Rukundo Placide ambaye ana Shahada ya Uzamivu katika uzalishaji wa mazao, amewataka wakulima wachangamkie kilimo cha viazi vitamu kama mkakati wa kuongeza usalama wa akiba ya chakula.

“Hakuna zao ambalo lina mavuno makubwa nchini Rwanda kama viazi vitamu maana kwenye shamba la heka moja unaweza ukavuna tani kati ya 15-30,” amesema.

Rukundo Placide, mtaalam wa viazi vitamu akiongea na Habari Pevu kuhusu umuhimu wa viazi vitamu kwenye jamii

Weka maoni