Wanawake wilayani Nyanza wataka Rais Kagame awe mgombea wao

269

Wanawake wilayani Nyanza nchini Rwanda wamemtumia ujumbe rais wa Rwanda Paul Kagame kuwa ndiye wanayemtaka awasimamie kwenye uchaguzi mkuu unaokaribia.

Vyama mbalimbali nchini Rwanda vinaendelea na zoezi la awali la kuchagua wagombea wao watakaowasimamia kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa Agosti 3-4, 2017.

Wanawake wilayani Nyanza wametoa ujumbe huo muda mfupi mara baada ya kumchagua bila kumpinga rais Paul Kagame, kuwa mwakilishi wao katika uchaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake, mmoja wao anayeonekana kwenye picha hapo juu, amesema wanawake wote wilayani Nyanza, watamchagua kwa asilimia mia kwa mia, na kwamba asiwe na wasiwasi kwani wako tayari kuunga mkono uongozi wake kwa muda wote atakaokuwa anawaongoza wanyarwanda.

Rais Kagame anayehitaji kuendelea kuiongoza nchi hii baada ya mihula yake miwili ya miaka saba saba kumalizika, wengi wanamsifia kwa kuwapa kipaumbele wanawake, hatua ambayo imelifanya taifa hili kuwa mstari wa mbele barani Afrika kwa kuonesha thabiti usawa wa kijinsia ndani ya utawala.

Hilo limethibitishwa na mama huyu mlemavu anayeonekana kwenye picha inayofuata juu ambaye amekiri kwamba Kagame hakuwasahau wanawake wanaoishi na ulemavu, kwani na wao wanathaminiwa sawa na wengine.

Kwa mantiki hiyo ni dhahiri kwamba, kama chama tawala nchini humu RPF kitamteua rais anayemaliza mihula yake miwili kuwa mgombea wake, huenda

kikashinda kwa kishindo cha juu kwenye uchaguzi ujao wa urais na kumpa fursa nyingine rais Paul Kagame ya kuliongoza taifa hili hadi mwaka 2024.

Weka maoni