Wanyarwanda 20 mbaroni Uganda

151
Hawa ni miongoni mwa Wanyarwanda waliotiwa mbaroni nchini Uganda wakisafiri kwenda Kampala

Raia 20 wa Rwanda wametiwa chini ya ulinzi nchini Uganda kwa madai ya kuingia nchini humo bila hati za usafiri.

Msemaji wa Jeshi ya Polisi katika eneo la Kigezi, Elly Maate, amesema ukamatwaji wa Wanyarwanda hao ni matunda ya juhuzi zilizofanywa na polisi walipoisimamisha basi katika manispaa ya Kabale.

Maate amesema abiria hao walikuwa wakisafiri kwenda mjini Kampala kwa basi la kampuni ya Baby Coach lenye namba ya usajili UAM 897C wakiwa hawana vitambulisho vya uraia wala hati za usafiri.

Afisa huyu wa usalama amewataka madereva kuchukua tahadhari wanapowaruhusu abiria waingie kwenye mabasi yao, kwani wengine huwa wana mipango ya kuhujumu usalama wa jamii.

“Madereva wanatakiwa wajihadhari na abiria wasiowajua kwani nchi yetu inataka kuimarisha usalama,” amesema Msemaji wa Jeshi la Polisi katika eneo la Kigezi.

Amuza Mugume, naibu mkuu wa kampuni ya usafiri wa umma ya Baby Coaches, amesema wanachoangalia ni kama abiria amelipa nauli na si vitambulisho vingine.

“Wamelipia usafiri kama abiria wengine, sikujua chochote kuhusu uwepo wapo nchini Uganda kinyume cha sheria,” amesema Mugume katika mahojiano na New Vision.

Mnamo Disemba 2016, Jeshi la Polisi la Uganda liliwarudishia Rwanda raia wake wapatao 41 ambao wamekamatwa wilayani Kabale wakiwa wameingia nchini humo kwa kuvunja sheria.

Wengi wa wahamiaji haramu hao ni wakazi wa Wilaya ya Burera ambao walidai walikwenda Uganda kwa lengo la kutafuta maisha katika mashamba ya vianzi mviringo.

Weka maoni