Wapiga kura njia panda wakati uchaguzi mkuu ukikaribia Rwanda

264
Rais Kagame anatarajiwa kugombea urais kusaka awamu ya tatu baada ya katiba ya nchi hii kurekebishwa mwaka 2015

Baadhi ya raia nchini Rwanda wako njia panda baada ya kushindwa kujua vituo vyao watakavyopigia kura.

Zimesalia siku sabini tu Wanyarwanda waanze kupiga kura kumchagua rais wao.

Maelekezo ya jinsi ya kujua kama jina la mpiga kura limeandikwa kwenye kitabu cha wapiga kura, jinsi ya kubaini kituo mtu atakachopigia kura na namna ya kuhama kituo cha kupigia kura, yako kwenye simu za mkononi.

Hata hivyo, wapo ambao hawajui kuangalia utaratibu huo kwa kutumia simu zao, hali ambayo imewapa wasiwasi hasa wale waliojiandikisha mahali tofauti na wanakofanyia kazi.

“Nilishiriki uchaguzi uliopita huko Kibuye magharibi mwa nchi hii, safari hii natamani nipige kura nikiwa hapa Kigali kwani ndipo ninapofanyia kazi siku hizi, tatizo sijui namna ya kuhama kituo wala kuangalia jina langu kwa kutumia simu hii,” amesema raia mmoja.

Mbali na hao wanaoshindwa kutumia simu zao, kuna kundi lingine la watu hususani wazee wasiotumia simu za mkononi, ambao na wao wanadai huenda wasiruhusiwe kupiga kura.

Katibu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi, Charles Munyaneza, amesema baada ya tatizo hilo kuonekana kuwa kikwazo siyo tu kwa wapiga kura bali hata kwa tume yake, wamekuja na jibu sahihi litakalowatoa tashwishwi wapiga kura hao.

“Tayari tumesambaza watu wa kujitolea kote nchini, huko vijijini ambako kuna idadi kubwa ya watu wasiojua kutumia simu, tumepeleka makaratasi na watu wako tayari kutazama majina yao kama yako kwenye orodha ya wapiga kura au la, na hata waliohamia mijini kama hawawezi kutumia simu wanaweza kufika katika ofisi zilizo karibu yao, ili wawasaidie kuhama vituo vya kupigia kura,” amesema Bw Munyaneza.

Uchaguzi Mkuu wa urais unatarajia Agosti 3, 2017 ambapo Wanyarwanda waishio nje watapiga kura kisha kesho yake yaani tarehe nne Wanyarwanda waishio nchini humu nao watadamkia vituoni kupiga kura wakimchagua rais wa nchi hii.

Weka maoni