Waziri Mkuu azipiga marufuku ibada za maofisini

124
Waziri Mkuu Anastase Murekezi

Waziri mkuu wa Rwanda, Anastase Murekezi, ameagiza watumishi wa umma waache mara moja ibada zinazofanyiwa maofisini na kuzorotesha utoaji wa huduma hasa mida ya mapumziko.

Agizo hilo limepigiwa debe na raia wengi wakisema walikuwa wamechoshwa na ibada hizo, huku wengine wakisema halina mantiki kwani mtu anahitaji kuomba Mungu muda wote kila anapotaka.

Janvier Ndayizeye ambaye ni Afisa Habari katika ofisi ya Waziri Mkuu, amesema si haramu kufanya ibada lakini watu wanatakiwa wajue kwamba ofisi ni sehemu za kazi na sehemu za ibada ni makanisa.

Wakati muda wa mapumziko kwa watumishi wa umma ukiwa ni saa sita mpaka saa saba za mchana, Ndayizeye amesema wapo ambao saa saba zikifika wanaendelea na ibada na kusababisha matatizo.

Amesema muda mwingine raia wakija kuomba huduma fulani hukosa mtu wa kuwahudumia kwani watumishi huwa wamejifungia maofisini wakipiga dua, na kusema tabia hiyo si ya kufumbia macho.

Aidha Bw Ndayizeye amedai ni dhahiri shahiri kuwa mtu akiombea ofisini huwapa wakati mgumu waumini wa madhehebu tofauti na ya kwake, na kusema hizo kero hazitakiwi ziendelee.

“Unaweza ukawa wewe ni Mkristo halafu unawazingua Waislamu, au tuseme wewe ni muumini wa ADEPR unawakera wenzio ambao si ADEPR,” amesema Bw Ndizeye.

Byiringiro Ally ambaye ni Muislamu ameelezea yaliyomsibu alipoenda sehemu fulani na kuwakuta watumishi wamejifungia ofisini wakifanya ibada huku wengine wakiwa wanakula chakula cha mchana.

“Nimewakuta baadhi wanapiga mlo wengine wanasali, ilibidi niketi niwasubiri mpaka walipotoka kwenye ibada ila hata walipotoka walikwenda kwenye mkutano, niliondoka bila kuhudumiwa.”

Ntwali Pie amesema kufanya ibada ni jambo jema ila “kila kitu kina muda wake, ukifungamanisha ibada na kazi ujue hapo unamdharau Mungu.”

“Hata kama Mungu ana muda wa kuwasikiliza wanawe, sidhani kama saa sita ndio muda mwafaka,” amesema Bw Ntwali.

Waziri Mkuu amewataka mawazili wote wafuatilie utekelezaji wa agizo hili ili asionekane tena mtu akiendesha shughuli za ibada katika sehemu za kazi.

Weka maoni