Waziri Mushikiwabo amkaba koo mkurugenzi wa Human Rights Watch

385
Waziri wa nchi wa nje wa Rwanda ambaye pia ni msemaji wa serikali Bi Louise Mushikiwabo (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch Kenneth Roth

Waziri wa nchi za nje wa Rwanda amemtaka mkurugenzi mtendaji wa Human Rights Watch aende kutafuta matibabu hospitali ya magonjwa ya akili.

Mahusiano baina ya Rwanda na shirika hilo la kimataifa la kupigania haki za binadamu (HRW) yanazidi kuwa mabaya.

Baada ya Rwanda kusitisha ushirikiano wake na shirika hilo mnamo Aprili 2017, pande mbili zimeendelea kurushiana matamshi makali.

Safari hii Katibu Mtendaji wa HRW Kenneth Roth, ameikosoa serikali ya Rwanda kwa kusema kuwa inawanyamazisha wapinzani wake kupitia hashtag ya #RwandaDecides kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

#RwandaDecides ni hashtag ambayo imekuwa ikitumiwa kuzungumzia mbio za urais ambapo Paul Kagame aliye madarakani tangu mwaka 2000 anasaka mhula wa tatu.

Kenneth Roth amesema #hashtag ya #RwandaDecides inatumika kuminya uhuru wa kujieleza kwa wakosoaji wa serikali ya Rwanda aliyoitaja kuwa ni ya wauaji.

Tweet hiyo ya Kenneth Roth iliwakera baadhi ya Wanyarwanda akiwemo waziri wa nchi za nje wa nchi hiyo ambaye pia ndiye msemaji wa serikali, Bi Louise Mushikiwabo.

“Ken, Ken, Ken, umetelekeza dawa yako tena? Rwanda kuna sehemu inaitwa Ndera ambapo unaweza kupata msaada!” imesema tweet ya Mushikiwabo.

CARAES Ndera ni hospitali maarufu sana nchini Rwanda ambapo hupelekwa wagonjwa wa mapungufu ya akili. Inapatikana jijini Kigali wilayani Gasabo.

Human Rights watch na mashirika mengine ya kimataifa pamoja na baadhi ya serikali za kimagharibi vimekemea mhula wa tatu wa rais Kagame tangu kipindi katiba ya jamhuri ya Rwanda ilipofanyiwa marekebisho kumwezesha rais Kagame kuwania awamu ya tatu.

Human Rights Watch imekuwa ikiituhumu serikali ya Rwanda kwa kutumia mabavu dhidi ya wapinzani huku ikiminya uhuru wa vyombo vya habari pia, madai ambayo serikali iliyatupilia mbali kwa nyakati tofauti.

Serikali ya Rwanda mwezi wa nne mwaka huu ilitangaza uamuzi wake wa kusitisha ushirikiano na Human Rights Watch (HRW) ambapo waziri wa Sheria Johnston Busingye ambaye ndiye Mwanasheria Mkuu pia, alisema hatua hiyo ilipigwa kufuatia shirika hilo kutoa ripoti zinazokinzana na maslahi ya Wanyarwanda.

“Tumeona ushirikiano wetu na HRW hautoi matunda, hauna tija, tumeona bora tuwaache waendelee kuandika wanavyotaka,” Busingye aliwaambia waandishi wa habari mjini Kigali.

“Hatuna kalamu zao, hatuna karatasi zao, ambacho tumeamua kuepuka ni kujibizana nao, hatutaki mawasilano nao,” aliongeza waziri Busingye.

Wanyarwanda leo tarehe 4 mwezi wa nane wamedamkia katika vituo vya kura kumchagua rais wa jamhuri ambapo wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wametabiri ushindi wa rais Kagame.

Weka maoni