Wema Sepetu ajisifia kuifufua Bongo Movie baada ya kifo cha Kanumba

401
Weme Sepetu amesema isingekuwa yeye Bongo Movie isingefufuka

Mrembo Wema Sepetu ambaye yupo nchini Rwanda tangia Jumatano wiki hii, amesema ndiye aliyeifufua tasnia ya Bongo Movie iliyokufa baada ya kifo cha Kanumba.

Amesema Kanumba alipofariki  hata Bongo Movie ilionekana imekufa kwani Kanumba alikuwa ndiye nguzo muhimu kwenye ramani ya filamu Tanzania.

Steven Meshaki Charles Kanumba almaarufu The Great Pioneer alifariki katika mazingira ya kutatanisha mnamo Aprili 2012 akiwa chumbani kwake na mpenzi wake Elisabeth Michael maarufu kama Lulu ambaye mwezi huu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua Kanumba bila kukusudia.

“Zamani Bongo Movie ilikuwa inafanya vizuri sana enzi za marehemu Steven Kanumba, alivyofariki kama na yenyewe ikafa. Tumekuwa tukiomboleza kifo chake na kifo chake kimetusababishia mazingira mabaya sisi kama waigizaji  kwa sababu tuko kwenye fani moja. Wengi wetu tumejikuta watu wanaona Bongo Movie haina mashiko,” amesema Wema katika mahojiano na waaandishi wa habari mjini Kigali.

Wema Sepetu akizungumzia alivyoirudisha ppazuri Bongo Movie iliyokuwa imelala baada ya kufariki Steven Kanumba

Ameongeza, “Kwa bahati nzuri mimi nimeweza kuileta tena Bongo Movie back to where it was (ilipokuwa enzi za Kanumba) baada ya kutoa filamu yangu ya Heaven Sent. Bongo Movie kama Bongo Movie zilikuwa zimelala kiukweli kabisa mpaka nilipozindua filamu yangu hiyo na nimeweza kuiweka kwenye application yangu kumekuwa kuna muhemko, yaani waigizaji wengi hata mkiwaona kwenye mitandao ya kijamii wanashoot, wanafanya vipindi, yaani Bongo Movie haijafa ni kazi nzuri tu tumeshindwa kuziweka sokoni. Tukiwa tuna kazi nzuri tukafanya vitu ambavyo vitapendwa na watu Bongo Movie itakuwa imara tena Inshallah!”

Mrembo huyo aliizindua filamu yake ya Heaven Sent Agosti 2017, ambapo alisema filamu hiyo ilimgharimu shilingi miliyoni 38. Alisema ni filamu nzuri kama zingine alizoachia awali, akijisifia kuwa hajawahi kutoa kazi mbovu.

Amekuja nchini Rwanda kwa ajili ya KFM Instagram Party, tamasha ambalo linatarajiwa kufanyika jioni ya leo (Ijumaa) katika viwanja vya Chillax Lounge vilivyo Nyarutarama, Kigali, masaa machache kabla ya yeye kupanda ndege kurudi Tanzania kesho asubuhi.

Wema Sepetu alianza kuigiza tangu akiwa shule ya msingi, lakini alikuja kuingizwa rasmi kwenye tasnia ya filamu na aliyekuwa mpenzi wake Steven Kanumba kipindi wakiwa na uhusiano.

Filamu ya Point of no Return aliyoigiza akiwa na Kanumba ndiyo iliyomfumbua macho na kumfanya atambue kipaji chake kilivyo kikubwa, na baada ya hapo ndipo akashiriki filamu mbalimbali zilizofanya vizuri ikiwemo Family Tears, Red Valentine na nyinginezo nyingi ambazo zilimvutia sifa ya muigizaji mzuri wa kike Tanzania.

Wema Sepetu aliwahi kutoka kimapenzi na marehemu Kanumba na Kanumba ndiye alimuingiza rasmi kwenye ulingo wa filamu

Weka maoni