Wimbo wa Bobi Wine unaomponda Museveni wapigwa marufuku

140
Bobi Wine (kushoto) na Rais Museveni

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Uganda (UCC) imepiga marufuku wimbo wa msanii Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’ ambao unamtuhumu Rais Museveni kwa kuongoza kimabavu.

Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, Bobi Wine aliendelea kuikosoa serikali ya Yoweli Kaguta Museveni ambaye amekuwa madarakani tangu Januari 1986.

Baada ya wimbo huo aliouachia Novemba 1, 2017 kupigwa marufuku, vyombo vya habari haviruhusiwi kuurusha na atakayethubutu kufanya hivyo ataadhibiwa vikali.

Chama tawala nchini Uganda cha NRM kiliahidi kuhakisha ibara ya 102 be ya katiba ya nchi hiyo inayomzuia mtu yoyote aliyetimiza umri wa miaka 75 kuwania madaraka ya urais inarekebishwa kwa ajili ya Museveni ambaye leo ana miaka 73.

Bobi Wine ameegemea upande wa upinzani. Yeye na wakosoaji wengine wa serikali wamesema watafanya kila lililo ndani ya uwezo wao kuhakikisha ibara hiyo inabaki ilivyo.

Katika wimbo wake huo anagusia vita ya kuikomboa Uganda ambayo Museveni alipigana dhidi ya Milton Obote miaka ya 80, ambayo ilimwingiza madarakani.

Kwa mujibu wa Bobi Wine, Museveni anafanya makosa aliyoyapiga vita. Bobi anaitaja serikali ya Museveni kuwa imewageuza wananchi kuwa watumwa nchini mwao.

Bobi amesema Museveni anawakandamiza wananchi wa Uganda kuliko weusi wa Afrika Kusini walivyokandamizwa enzi za za ubaguzi wa rangi wa Apartheid.

“Vita ya ukombozi ililenga nini kama leo hatuwezi kushuhudia makabidhiano ya madaraka katika hali ya amani? Nini umuhimu wa katiba kama serikali inapuuza katiba?” anahoji Bobi Wine.

“Uhuru wa kuongea uko wapi kama unanipandisha kizimbani kisa nimejieleza?”

“Unachokifanya unadhani unatoa somo gani kwa vizazi vijavyo,” Bobi amuuliza Museveni.

Bobi Wine ambaye alizaliwa mwaka 1982, ameingia bungeni Julai 1, 2017 akiwakilisha jimbo la Kyaddondo Mashariki lililoko Wilaya ya Wakiso.

Amekuwa akiiponda serikali ya Rais Museveni na kuwataka raia kupambana na rushwa anayoitaja kuwa ni miongoni mwa vyanzo vya kuzorota kwa maendeleo ya taifa hilo.

Juzijuzi alidai kukataa kupokea mamiliyoni ya shilingi yalichoingizwa kama hongo kwenye akaunti yake ya benki kumtaka aridhie muswada wa sheria unaolenga kumwezesha Museveni kugombea mhula mwingine.

Weka maoni