Yanga walaani kitendo cha mashabiki kuchoma jezi ya Haruna Niyonzima

285
Haruna Niyonzima uwanjani

Uongozi wa klabu ya Yanga umelaani vikali kitendo cha mashabiki wachache wa klabu hiyo kuchoma jezi namba 8 iliyokuwa inavaliwa na kiungo Haruna Niyonzima.

Kupitia kwa katibu mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema mashabiki wanapaswa kujitambua kwani Niyonzima sio mchezaji wa kwanza kuondoka klabuni na kitendo cha kuchoma jezi ni ishara ya kukosa uungwana, kwa mujibu wa Bongo5.

Sio sahihi, huwezi kuchoma jezi ya mtu heti kisa kaondoka, Niyonzima sio mchezaji wa kwanza kuondoka au kujiunga na Yanga. Mashabiki wanapaswa kujitambua na kuelewa mchezo wa soka uko vipi, sisi tunaona hili si jambo la kiungwana,” alisema Mkwasa.

Katibu mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Boniface Mkwasa

Wiki iliyopita Yanga ilitangaza rasmi kumuachia Niyonzima kuendelea na maisha yake ya soka nje ya Yanga ya baada ya kushindwana kwenye makubaliano ya malipo.

Siku chache baada ya kauli hiyo, ikaonekana baadhi ya mashabiki wakichoma jezi za kiungo huyo Mnyarwanda wakionyesha hasira zao kutokana na uamuzi wake wa kuondoka na kuanza mazungumzo na Simba.

Hata kabla ya uongozi wa Yanga kutamka kuhusiana na tukio hilo, baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao wengi wanajitambua pia walilaani tukio hilo na kuliita ni la kishamba.

Weka maoni