Yvonne Chaka Chaka kutua Rwanda wiki hii

400
Yvonne Chaka Chaka

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Afrika Kusini Yvonne Machaka almaarufu Yvonne Chaka Chaka anatarajiwa kurudi nchini Rwanda kwa ajili ya sherehe za shirika la Global Fund.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, ‘Malkia wa Afrika’ amesema atawasili Mjini Kigali siku ya Alhamisi kuadhimisha maisha ya watu miliyoni 20 yaliyookolewa duniani kote.

Amewataja watu hao kuwa walikuwa wanasumbuliwa na magonjwa ya ukimwi, maleria na kifua kikuu. Utakuwa pia ni muda mwafaka wa kushuhudia mafanikio ya Rwanda katika sekta ya afya.

Yvonne Chakachaka, 52, anatunga na kuimba nyimbo, lakini pia ni mjarisiamali na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini. Ni msanii anayeheshimika nchini humo tangu mwaka 1990.

Album yake ya kwanza inaitwa ‘I’m in Love With a DJ’. Nyimbo kama ‘I’m burning up’, “I Cry for Freedom”, “Umqombothi” ni miongoni mwa zile zilizomzolea umaarufu wa kimataifa.

Aliwatumbuiza Malkia wa Uingereza Elizabeth II na Bill Clinton alipokuwa Rais wa Marekani.

Yvonne Chaka Chaka akiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame na mkewe Jeannette Kagame siku za nyuma alipokuwa nchini Rwanda

Mwaka 2011 alikuja Rwanda ambapo, akishirikiana na Mke wa Rais wa Rwanda Jeannette Kagame, waliwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililoukumba Mkoa wa Kaskazini.

Mwaka 2007 pia alikuwa Rwanda alipofanya tamasha la kihistoria Jijini Kigali. Aliwaacha hoi mashabiki wake katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuundwa kwa Mji wa Kigali.

Chaka Chaka ni Balozi wa Shirika la Kimataifa la Global Fund linalojishughulisha na masuala ya afya, ambapo anajihusisha sana na kupambana na ukimwi, kifua kikuu na malaria.

Aliteuliwa na Marehemu Nelson Mandela kuwa Balozi wa Mfuko wa watoto wake.

Aliunda mfuko wake mwenyewe wa Princess of Africa Foundation akitumia jina hilo la umalkia alilopewa nchini Uganda mnamo mwaka 1990.

Chaka Chaka alizaliwa Dobsonville huko Soweto, nchini Afrika Kusini mwaka 1965.

Weka maoni