Zimamoto refu zaidi Afrika lazinduliwa Rwanda

850
Gari la kisasa la kuzima moto la Jeshi la Polisi la Rwanda

Polisi nchini Rwanda imeonesha gari refu kuliko magari yote barani Afrika yanayofanya kazi ya kuzima moto juu ya maghorofa marefu.

Kwa mujibu wa kamanda wa kikosi cha zima moto nchini humu, ACP Jean Baptist Seminega, hakuna jengo la ghorofa hata moja jijini hapa ambalo ni refu kuliko gari hilo.

Amesema kuna uwezekano mkubwa wa kukabiliana na ajali ya moto inayoweza kuyakabili majengo marefu jijini hapa.

Zimamoto hilo ndilo gari refu kuliko magari yote barani humu, kwani lina urefu wa mita 53.

“Gari hili ndilo gari la kuzima moto ambalo ni refu kuliko magari yote barani Afrika, wanaotufuata ni Misri wenyewe wana gari lenye urefu wa mita 40, Afrika ya kusini ni wa tatu baada ya misri kwa kuwa na gari refu la kuzima moto, ni gari la kisasa lenye uwezo wa kuzima moto juu ya maghorofa marefu,” amesema ACP Jean Baptiste.

Gari la zimamoto la Rwanda

Hata hivyo jeshi la polisi kikosi cha zimamoto linadai pamoja na kuwa na vifaa hivyo vya kisasa, lakini havitoshi kwani siyo kila wilaya nchini humu ina gari la kuzima moto.

“Vifaa tunavyo ndiyo lakini siyo kila jimbo, wilaya na hata tarafa, ina vifaa hivi, mradi tayari tumeshauandaa lakini bado hatuanza kununua magari ya zimamoto yatakayopelekwa katika kila kona ya nchi hii,” ameongeza ACP Jean Baptiste Seminega.

Rwanda ni miongoni mwa nchi mbalimbali barani Afrika ambazo baadhi ya maeneo yake yakiwemo majengo, maghala, viwanda na hata nyumba binafsi yamekuwa yakikumbwa na ajali za moto, hivyo ujio wa gari hilo watajwa kuwa mkombozi wa kuweza kukabiliana na ajali kadha wa kadha.

Ikumbukwe miezi miwili iliyopita, baadhi ya maeneo ya Gereza la Gasabo yaliungua kiasi ambacho baadhi ya vifaa vya wafungwa katika eneo lililokumbwa na ajali hiyo viliungua na kusababisha hasara kubwa kwa wafungwa na serikali zima kwa ujumla.

Weka maoni